Wewe ni nani?DP Gachagua amuuliza Raila huku akiendelea kumtupia makombora

DP Gachagua alisema kuwa hakuna nafasi ya Odinga kutoa matakwa kwa serikali tawala

Muhtasari
  • DP Gachagua vile vile alimtaja Odinga kwa kuwa mhimili mkuu wa serikali ya hendisheki chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.
DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
Image: Facebook, Maktaba

Naibu Rais Rigathi Gachagua amemkashifu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa madai ya kuingilia masuala ya utawala wa Kenya Kwanza.

Hii ni baada ya Odinga Alhamisi kutoa orodha ya matakwa kumi kwa Rais William Ruto akiangazia jinsi kiongozi huyo wa nchi anapaswa kupunguza matumizi ya serikali na kuwarahisishia Wakenya gharama ya maisha.

Akizungumza katika Kaunti ya Meru mnamo Ijumaa, DP Gachagua alisema kuwa hakuna nafasi ya Odinga kutoa matakwa kwa serikali tawala zaidi akibainisha kuwa kiongozi huyo wa upinzani anafaa kuheshimu matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 2023 ambao ulishuhudia Rais Ruto akikalia nyumba ya mlima. .

"Ati amepeana matakwa? Amepeana matakwa kwa nani? Umechaguliwa na nani? Wewe ni nani kwa Kenya? Si ungojee 2027 unakuja kuwashawishi hawa watu waje kukupa fursa," alisema Gachagua.

DP Gachagua vile vile alimtaja Odinga kwa kuwa mhimili mkuu wa serikali ya hendisheki chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Gachagua anasema Odinga alipata fursa ya kuanzisha mageuzi, kama yale aliyopendekeza kwa Rais Ruto, wakati Uhuru akiwa mamlakani lakini akachagua kutofanya hivyo kwa maslahi yake binafsi.

"Wewe ulikuwa kwa serikali ya Uhuru Kenyatta na ulikuwa mshauri. Ungechangia hivyo maneno unasema lakini haukufanya lolote. Ulituachia nchi ambayo imesambaratika na ukaharibu ajenda ya Jubilee. Ulisimamisha makazi, ukasimamisha huduma ya afya kwa wote na ukatupeleka katika miradi isiyo na maana kama BBI," Gachagua alisema.