Mkewe Boni Khalwale afanyiwa upasuaji wa kubadilisha goti, seneta huyo afurahi

Kwa Khalwale, taarifa zozote zenye ufanisi katika familia yake, ziwe ndogo ama kubwa ni kawaida yake kuzishiriki kwa wafuasi wake mitandaoni, ikiwa ni pamoja na wanawe wanapopasi mitihani, mbuzi kujifungua mtoto, n.k

Muhtasari

• Kupitia ukurasa wake wa X, awali ukijulikana kama Twitter, Khalwale ambaye pia ni daktari wa upasuaji aliwashukuru madaktari hao.

Boni Khalwale afurahi mkewe kufanyiwa upasuaji
Boni Khalwale afurahi mkewe kufanyiwa upasuaji
Image: Twitter

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ametoa shukrani sufufu kwa timu ya madaktari katika hospitali ya Agha Khan kwa kufanikisha shughuli nzito ya kumfanyia mkewe upasuaji wa goti.

Kupitia ukurasa wake wa X, awali ukijulikana kama Twitter, Khalwale ambaye pia ni daktari wa upasuaji aliwashukuru madaktari hao akisema kwamba baada ya mchakato huo mgumu uliochukua saa kadhaa, hatimaye mkewe sasa yuko vizuri na anaendelea kupata nafuu.

Mkewe Khalwale alikuwa anafanyiwa upasuaji wa kubadilisha kabisa goti la mguu wake wa kulia.

“Asante, mwenzangu na rafiki Dkt Opondi, timu nzima ya upasuaji, na Hospitali ya Aga Khan kwa upasuaji uliofaulu kwa mke wangu. Mama Josephine Umina Khalwale yuko katika furaha anapopata nafuu kutokana na upasuaji wa Kubadilisha goti. Tuna furaha!” alichapisha Khalwale.

Khalwale alipakia picha za mkewe akiwa kitandani na pia mguu uliofanyiwa upasuaji kitendo ambacho kiliwaudhu baadhi ya watu ambao walisema ni kinyume na maadili ya kijamii mtu kuchapisha picha za mgonjwa akiwa katika hali ya kutojitambua mitandaoni.

“Ni wakati wa kuzungumza juu ya faragha ya mgonjwa. Ukweli kwamba yeye ni mke wako haukupi haki ya kuchapisha picha zake kwenye Twitter. Je, wewe si mtaalamu wa matibabu?” mtumizi mmoja kwa jina Abiuth Maronga alisema.

“Why post this though....ama unataka sympathy...” Stephen Paul alimuuliza.

“Kupiga picha za wagonjwa katika kitanda cha hospitali na kuzishiriki hadharani ni kinyume cha maadili na sio kitaalamu zaidi kutoka kwa mtu anayejifanya kuwa daktari. QR kwa mama,” Reuben Musazia alisema.

Lakini kwa wale wanaomjua Khalwale, ni mtu ambaye huwa na furaha sana kuonesha kila mafanikio madogo kwa makubwa kwenye familia yake mitandaoni.

Kutoka kwa  watoto wake kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitafia, yeye kusafiri kwa ndege hadi wakati mbuzi wake anapojifungua mtoto, kwa Khalwale hizo ni taarifa kubwa sana ambazo wafuasi wake mitandaoni wanastahili kuzijua.

Maoni yako ni yepi?