Mhudumu wa kituo cha petroli atekwa nyara na kutupwa nje ya gari likienda kasi

Kulingana na ripoti, mhudumu huyo alitekwa nyara na watu wasiojulikana ambao walikuwa wametoka kujaza mafuta katika kituo cha mafuta alichokuwa akisimamia

Muhtasari

• Mhudumu huyo aliokolewa na raia wema na askari polisi wa Kangundo waliompata barabarani akiwa na majeraha na kumpeleka hospitalini.

Crime Scene
Image: HISANI

Mhudumu wa kituo cha mafuta ya petroli alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Kangundo baada ya kurushwa nje ya gari lililokuwa likiendeshwa siku ya Jumatatu, Citizen wameripoti.

Kulingana na ripoti, mhudumu huyo alitekwa nyara na watu wasiojulikana ambao walikuwa wametoka kujaza mafuta katika kituo cha mafuta alichokuwa akisimamia kando ya barabara ya Tala-Kangundo.

Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kupaka mafuta waligoma kulipwa fedha zao na badala yake walishuka na kumlazimisha mhudumu huyo kuingia ndani ya gari kabla ya kuondoka kwa kasi.

Watu waliokuwa ndani ya gari hilo aina ya Toyota Probox inasemekana kuwa walimtupa nje ya gari lililokuwa likienda kabla ya kuondoka tena kwa kasi.

Mhudumu huyo aliokolewa na raia wema na askari polisi wa Kangundo waliompata barabarani akiwa na majeraha na kumpeleka hospitalini.

Aliaga dunia katika hospitali ya Kangundo, na mwili wake kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo hicho.