Wasomali wenye ualbino: Wanaopigwa mawe na mayai

"Tulitukanwa na kuteswa kila mara na jamii yetu. Tulipigwa na kukejeliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi, nywele na macho yetu," anasema.

Muhtasari

• "Nilidhani ningepata maisha bora huko Mogadishu lakini nilikosea."

• Bw Mohamed alitafuta na kutafuta chumba katika nyumba ya pamoja lakini alikataliwa kila kona.

NAAIMA SAED SALAH
NAAIMA SAED SALAH
Image: BBC NEWS

Akirejelea unyanyapaa anaokabiliana nao nchini Somalia kwa sababu ana ulemavu wa ngozi, Elmi Bile Mohamed mwenye umri wa miaka 25 anasema: "Watu huniambia mimi ni mla watu na nitakula watoto wao. Wananiogopa."

Bw Mohamed ametatizika kupata mahali pa kuishi katika mji mkuu, Mogadishu, tangu aondoke nyumbani kwake kijijini katika eneo la kati la Hiraan. Ndugu zake pia wanakabiliwa na hali hiyo.

"Tulitukanwa na kuteswa kila mara na jamii yetu. Tulipigwa na kukejeliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi, nywele na macho yetu," anasema.

"Nilidhani ningepata maisha bora huko Mogadishu lakini nilikosea."

Bw Mohamed alitafuta na kutafuta chumba katika nyumba ya pamoja lakini alikataliwa kila kona.

Aliishia kulipa $30 (£23) kwa mwezi kuishi katika ghala katika wilaya ya Hamar Weyne, sehemu kongwe zaidi ya jiji hilo.

"Watu wanadhani nimelaaniwa," anasema. "Mara nyingi watu hutupa mchanganyiko wa maji ya chumvi na mayai mabichi kwenye mlango wangu kwa sababu wanaamini kuwa hii itawalinda na mimi."

Hatimaye Bw Mohamed alipata kazi ya kusafisha katika mkahawa mmoja akipata kati ya $1.40 na $4 (£3) kwa siku.

Haikuchukua muda mrefu.

Alifukuzwa kazi baada ya wateja kuacha kwenda kula chakula huko, wakisema wanahofia angewaambukiza ualbino ingawa sio ugonjwa wa kuambukiza, bali ni maumbile.

"Nilienda kutoka mgahawa hadi mgahawa nikitafuta kazi nyingine lakini hakuna mtu angeniajiri," asema. "Niliishia kuomba mitaani, huku nikishikilia bango lenye nambari yangu ya simu ili watu watoe michango kupitia malipo ya simu."

Pesa anazopata kutokana na kuombaomba hazitoshi kulipia milo yake na kukodisha, achilia mbali kinga ya jua na miwani anayohitaji ili kulinda ngozi na macho yake nyeti.

Watu wenye ualbino wana rangi ya mwili ( melanini) kidogo au hawana kabisa, rangi inayopaka macho, nywele na ngozi na kuwalinda dhidi ya jua.

Pesa anazopata kutokana na kuombaomba hazitoshi kulipia milo yake na kukodisha, achilia mbali kinga ya jua na miwani anayohitaji ili kulinda ngozi na macho yake nyeti. Watu wenye ualbino wana melanini kidogo au hawana kabisa, rangi inayopaka macho, nywele na ngozi na kuwalinda dhidi ya jua.

"Sina uwezo wa kununua miwani," Bw Mohamed anasema. "Kuna vumbi jingi na msongamano wa magari unaochafua sana sokoni ambako ninaomba.

Macho yangu yana uchungu kila mara na uwezo wa kuona kwangu unazidi kuzorota kwa kasi."

"Wakati mwingine watu hunipa mabaki yao ili nile. Wakati mwingine sina chochote."

Ndoto za Bw Mohamed za kukimbilia Mogadishu kutafuta pesa za kurudisha familia yake, hasa ndugu zake albino, zimekatizwa.

Haijabainika ni watu wangapi wenye ualbino wanaishi Somalia kwani hakuna data inayopatikana. Nchi imeathiriwa na migogoro na ukosefu wa utulivu kwa zaidi ya miongo mitatu hivyo haiwezekani kukusanya taarifa za uhakika.

Mapema mwaka huu, takriban familia 80 zinazoishi na ualbino huko Mogadishu ziliungana na kuunda chama, Albino wa Somalia, ambacho wanatumaini kitaongeza ufahamu kuhusu masaibu yao na kusaidia kupunguza unyanyapaa.

Kufikia sasa, wametumiwa chupa 86 za mafuta ya jua kutoka kwa wanawake wa Kisomali wanaoishi ughaibuni.

Inapendekezwa kuwa watu wenye ualbino wavae mafuta ya kujikinga na jua, mavazi ya kujikinga na miwani ili kupunguza mionzi ya jua.

Ukosefu wao wa melanini unamaanisha kuwa wako kwenye hatari kubwa ya kupata kuchomwa na jua na saratani ya ngozi.

Pia husababisha matatizo ya macho kwani melanin inahusika katika ukuzaji wa retina, safu nyembamba ya seli nyuma ya jicho.

"Wasomali wengine wenye ulemavu wameunda mashirika ambayo yanashawishi msaada kutoka kwa serikali na mashirika ya kimataifa," anasema mwenyekiti wa kikundi hicho, Mohamed Abukar Abdiqadir mwenye umri wa miaka 40. "Sasa wana haki. Hatuna."

“Nilichaguliwa kuwa kiongozi wa chama chetu kwa sababu mimi ni shujaa na huwa sikati tamaa,” asema Bw Abdiqadir, ambaye ana watoto sita. Kama yeye, wote wanaishi na ualbino.

Anatafuta riziki kwa kuuza vyakula vilivyokaushwa na vya bati kutoka kwa toroli katika soko la Hamar Weyne. Daima huvaa kofia ili kujikinga na jua kali.

"Sababu ya watu kutuchukia na kutuogopa ni ujinga," anasema.

"Uovu na ubaguzi tunaokabiliana nao lazima usituzuie kupigania haki zetu na kulisha familia zetu. Ikiwa Wasomali watajifunza kuhusu ualbino, watatambua sisi ni watu kama wao."

Kwa sasa, chuki dhidi ya watu wenye ualbino ni mbaya sana hivi kwamba watoto walio na ugonjwa huo ni nadra sana kupata elimu.

“Niliwatoa watoto wangu shuleni kwa sababu walikuwa wakipigwa mawe kila siku,” anasema Asha Gele, ambaye wanawe wawili wanaishi na ualbino.

“Ngozi yao dhaifu iliharibiwa vibaya na mawe waliyorushiwa na watu, kwa hiyo sasa ninawaweka ndani siku nzima, kila siku,” anasema. "Hawatapata elimu, hawatajifunza kucheza na watoto wengine, lakini angalau watakuwa salama."

Familia inalipa dola 40 kwa mwezi kuishi katika nyumba ya muda ya vyumba viwili katika wilaya ya Huriwa kaskazini mwa Mogadishu.

Kuta zake na paa zimejengwa kutoka kwa nguo kuukuu na karatasi zilizovunjika, zilizo na kutu za bati, hazitoshi kuzuia mwanga wa jua kuingia na kuchoma ngozi ya watoto.

"Nilikuwa nikipata pesa nzuri kwa kuuza mboga sokoni," Bi Gele anasema. "Ilinibidi niache biashara yangu ili nibaki nyumbani na watoto wangu. Sasa tunatatizika kuishi kwa dola 4 hadi 6 ambazo mume wangu hupata kila siku kama dereva wa riksho."

Bi Gele anasema ndoa yake inasambaratika kwa sababu mumewe anamlaumu kwa kuzaa watoto wenye ualbino. Anamshutumu kwa kuleta bahati mbaya kwa familia.

"Watu ninaowapenda zaidi - mume wangu na jamaa zangu - wanawaepuka watoto wangu. Kaka yangu mwenyewe anajiweka mbali kwa sababu anaamini watamambukiza ualbino," anasema.

"Lakini siku zote nitasimama na kuwatetea hata iweje. Nitavumilia na sitawapuuza kamwe. Hawakuchagua kuishi hivi."