Ruto adai makamu wa rais wa Kolombia ana usuli wa Kenya, amuita Nyawira kutoka Meru

"Na kusema kweli Francia ana jina la Kikenya, anaitwa Nyawira na alipokuja Kenya tulifuatilia usuli wake mpaka sehemu inayoitwa Meru" - Ruto aliwaambia wageni.

Muhtasari

• Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa Mina kuzuru Kenya.

• Mina alionekana mrembo akiwa amevalia vazi la mauve alipokuwa akiwahutubia wajumbe kwa Kihispania.

Makamu wa rais wa Kolombia Francia Mina na rais wa Kenya William Ruto.
Makamu wa rais wa Kolombia Francia Mina na rais wa Kenya William Ruto.
Image: Facebook

Ikiwa ni siku ya tatu ya kongamano la kilele cha hali ya hewa jijini Nairobi Kenya, jiji hili limeshuhudia viongozi wa matabaka mbali mbali kutoka kote ulimwenguni wakifurika ili kuhudhuria na kutoa hamasa kuhusu hali ya hewa.

Mmoja wa wageni waliohudhuria kongamano hilo ni naibu wa rais wa taifa la Kolombia Francia Mina.

Mina, ambaye asili yake ni ya Kiafrika alitajwa na rais Ruto katika kongamano hilo kama Mtu mwenye usuli wake nchini Kenya, akienda hata Zaidi na kusema kwamba jina lake la Kikenya ni Nyawira kutoka kaunti ya Meru.

Mina alionekana mrembo akiwa amevalia vazi la mauve alipokuwa akiwahutubia wajumbe kwa Kihispania huku mkalimani akimsaidia kupitisha ujumbe wake kwa Kiingereza.

Hata hivyo, mara tu alipomaliza hotuba yake, Ruto, ambaye alikuwa kwenye jukwaa akisimamia kikao, alimshukuru na kufichua kwamba kiongozi huyo wa Colombia ana asili yake nchini Kenya.

“Ahsante sana dadangu Francia kwa hotuba hiyo ya kiuhakika. Na kusema kweli Francia ana jina la Kikenya, anaitwa Nyawira na alipokuja Kenya tulifuatilia usuli wake mpaka sehemu inayoitwa Meru. Kwa hiyo ahsante sana Nyawira,” Ruto alisema huku akimkaribisha mgeni mwingine jukwaani kutoa hotuba yake.

Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa Mina kuzuru Kenya.

Mwezi Mei alizuru Kenya na alionekana akiwa na naibu rais Rigathi Gachagua ambapo walifanya mazungumzo ya kina kuhusu jinsi ya kuboresha hata Zaidi uhusiano baina ya mataifa haya mawili.