World Coin: Waliofanyiwa 'scanning' ya mboni za macho wakiri kupata matatizo ya kuona

" Tatizo hilo lilianza kama saa mbili baada ya kuchanganuliwa macho na limekuwa likiendelea" Mogusu, mmoja wa waatrhirika alikiri.

Muhtasari

• Mwathirika mwingine kwa jina Bernard Ayoo alisema alikuwa katika mradi huo kwa ajili ya kupata pesa lakini akakiri kwamba alilaghaiwa baadae.

Mwathirika wa World Coin.
Mwathirika wa World Coin.
Image: Star, Screengrab

Baadhi ya Wakenya waliokubali kumulikwa macho yao na kamera ya kuchanganua macho mwishoni mwa mwezi Julai jijini Nairobi na mawakala wa World Coin sasa wamejitokeza na kukiri kwamba wamekumbwa na matatizo ya kuona.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopeperushwa katika runinga ya Citizen usiku wa Jumanne, baadhi ya waliokubali kuchanganuliwa macho kwa ajili ya kulipwa shilingi elfu 7 za Kenya wamekiri kupatwa na matatizo mbalimbali ya macho.

Akitoa ushuhuda wake mbele ya kamati ya muda ya bunge ambayo ilitengenezwa kuchunguza shughuli za World Coin nchini Kenya, Marube Mogus – mmoja wa waliochanganuliwa macho alikiri kwamba amepata matatizo ya kuona.

“Macho yangu yalionekana kuathirika kutokana na miale ya UV, na yalianza kuwa na machozi na pia kuwashwa. Tatizo hilo lilianza kama saa mbili baada ya kuchanganuliwa macho na limekuwa likiendelea. Kusema kweli mpaka sasa nimeshaenda hospitalini na nimeelewa kutumia miwani,” Mogusu alisema.

Mwathirika mwingine kwa jina Bernard Ayoo alisema alikuwa katika mradi huo kwa ajili ya kupata pesa lakini akakiri kwamba alilaghaiwa baadae.

“Ndio nilipata baadhi ya pesa lakini si kiwango ambacho walikuwa wametuahidi. Waliniambia wangenipa shilingi elfu 7 lakini nilipata shilingi elfu 2 pekee,” alisema.

Mwathirika mwingine ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu aliambia kamati hiyo kwamba hakukuwa na mkataba wa maelewano baina ya mawakala wa World Coin na waliokuwa wakichanganuliwa macho.

“Jamaa huyo aliniambia kwamba walikuwa wanafanya scanning kwa ajili ya World Coin, aliniambia kwamba baada ya kuchanganuliwa mboni ya jicho nitapata takrima ya dola 70. Mara ya kwanza nilikuwa na woga lakini baada ya kusema kwamba nitapata pesa, nilikubali,” alisema.

Wengi wa vijana waliofanyiwa uchanganuzi wa mboni za macho wanasema wanapitia unyanyapaa kutoka kwa marafiki wenzao ambao hawakufanyiwa scanning.

Kamati hiyo ya bunge inalenga kutathmini uhusiano uliopo kati ya biashara ya fedha na biashara ya World Coin, haswa wakilenga kubaini chanzo cha pesa ambazo walikuwa wakiwapa watu kwa ajili ya kufanyiwa scanning ya mboni za macho yao.