Familia za wahanga wa Shakahola zasusia kutoa maiti mochwari kisa hofu ya uchawi

Hadi sasa, serikali imefukua miili 429 kutoka Msitu wa Shakahola. Inaaminika kuwa wahasiriwa hao walivurugwa akili na Mackenzie, ambaye aliwataka wafe njaa ili wakutane na Mungu.

Muhtasari

• "Wengine wanaamini jamaa zao wangeweza kushiriki katika uchawi na kafara za binadamu, na familia za wahasiriwa pia zinakabiliwa na unyanyapaa," aliongeza.

• Inaarifiwa kwamba familia hizo sasa zinahofia kuandamwa na mizimu iwapo watakwenda kuichukua miili ya wapendwa wao.

Image: MAKTABA

Ikiwa ni miezi kadhaa baada ya hofu ya Shakahola kutanda kote ulimwenguni baada ya kubaini kwamba shamba la mchungaji mwenye utata Paul Mackenzi lenye upana wa ekari 800 lilikuwa ni makaburi ya halaiki kwa waumini wa kanisa lake, sasa imebainika kwamba familia za wahanga hao zimesusia kutoa maiti za wapendwa wao katika vyumba vya kuhifadhi maiti.

Kwa mujibu wa ripoti ya runinga ya Citizen TV, baada ya miili Zaidi ya 400 kufukuliwa kutoka kwa makaburi hayo ya halaiki huko Shakahola kaunti ya Kilifi, umepita muda mrefu bila wapendwa wao kufika katika hifadhi za maiti maiti hizo zilikohifadhiwa ili kuichukua na kuwapa heshima za mwisho.

Inaarifiwa kwamba familia hizo sasa zinahofia kuandamwa na mizimu iwapo watakwenda kuichukua miili ya wapendwa wao.

“Baadhi ya familia hawataki kuchukua miili kwa ajili ya kuzikwa katika nyumba zao, bado tutalazimika kuzitafuta familia hizi kwa sababu tunahitaji ridhaa yao kuzika maiti huko Shakahola au sehemu nyingine ambayo itakuwa imetengwa na serikali," Mkurugenzi wa Haki Africa Mathias Shipeta alisema.

 "Wengine wanaamini jamaa zao wangeweza kushiriki katika uchawi na kafara za binadamu, na familia za wahasiriwa pia zinakabiliwa na unyanyapaa," aliongeza.

Hadi sasa, serikali imefukua miili 429 kutoka Msitu wa Shakahola. Inaaminika kuwa wahasiriwa hao walivurugwa akili na Mackenzie, ambaye aliwataka wafe njaa ili wakutane na Mungu.