Ruto alalamika rais wa TZ kutumia neno 'Azimio' katika hotuba yake mara kwa mara - Video

"Nimesikia kwa taarifa yako umerudia Azimio, Azimio, Azimio, hawa watu walikuwa na Azimio. Sasa nikapata kidogo wasiwasi kwa sababu kule kwetu Azimio ni mambo mengine. Azimio ni chama cha upinzani kiko na fujo kweli,” Ruto alisema.

Muhtasari

• “Lakini hata hivyo nimeelewa kwamba kumbe Azimio inaweza kuwa ni mambo mazuri ya makubaliano,” aliongeza rais Ruto.

Marais wa Kenya na Tanzania, Ruto na Hassan.
Marais wa Kenya na Tanzania, Ruto na Hassan.
Image: Facebook

Rais wa Kenya William Ruto amemlalami,ia kwa njia ya utani mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutumia msamiati wa baadhi ya maneno ambayo humu nchini yanalenga Zaidi upande wa kisiasa.

Akizungumza na wajumbe kwa lugha ya Kiswahili, Ruto alisema kwamba alimsikia Suluhu akitumia baadhi ya misamiati ya Kiswahili ambayo kwa muktadha wa siasa za Kenya inaegemea mirengo mbali mbali ya kisiasa, akisema kwamba kidogo aliingiwa na wasiwasi.

Ruto alimtania Suluhu kwamba alimsikia katika hotuba yake akitumia neno ‘Azimio’ mara Zaidi ya moja na karibia aingiwe na wasiwasi kwa kudhani kwamba kiongozi huyo alikuwa anapigia debe mrengo wa upinzani wa humu nchini Azimio la Umoja.

“Lakini niko na malalamiko kidogo, wacha niseme. Kwamba, pia nimesikia kwa taarifa yako umerudia Azimio, Azimio, Azimio, hawa watu walikuwa na Azimio. Sasa nikapata kidogo wasiwasi kwa sababu kule kwetu Azimio ni mambo mengine. Azimio ni chama cha upinzani kiko na fujo kweli,” Ruto alisema huku wajumbe Tanzania wakiangua kicheko.

Rais Ruto hata hivyo alisema kwamba baada ya kusikiliza muktadha, alielewa kwamba Azimio kumbe kwa upande mwingine linaweza kuwa ni jambo zuri.

“Lakini hata hivyo nimeelewa kwamba kumbe Azimio inaweza kuwa ni mambo mazuri ya makubaliano,” aliongeza rais Ruto.

Tazama video hii hapa chini;