Eti mlienda kutafuta maendeleo ikulu, maendeleo ya mamako - Raila kwa wabunge waasi

Waliofukuzwa ni pamoja na mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, mbunge wa Suba ya Kusini Caroli Omondi, mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o, mbunge wa Bondo Gideon Ochanda na seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Muhtasari

• Siku mbili zilizopita, ODM ilitoa barua ikieleza kufukuzwa kwa wabunge wanne na seneta mmoja ambao walikutana na Ruto katika ikulu.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Facebook

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amewataka wabunge na maseneta waasi wa chama hicho waliokutana na rais Ruto katika ikulu ya Nairobi kujiuzulu ili nyadhifa zao kutangazwa wazi kwa ajili ya uchaguzi mpya.

Akizungumza Ijumaa, Odinga alisema kwamba wabunge hao waliofukuzwa chamani walifanyiwa hivyo baada ya kukiuka sera na kanuni za chama.

Aliwasuta kwa kujitetea kwamba walikwenda katika ikulu ya Nairobi kutafuta maendeleo, akisema kwamba katika katiba mpya ya Kenya, maendeleo huratibiwa na bunge wala si ikulu.

“Sasa wewe unajitokeza kisirisiri usiku unasikia ati nimeitwa sijui na nani, waziri Fulani, eti mnaenda ikulu. Hakuna mtu anataka usiende ikulu, lakini unaambia chama mimi nimealikwa kule ili tushauriane,” Odinga alisema.

“Unaenda kufanya nini, eti mimi naenda kutafuta maendeleo. Maendeleo ya mama yako? Kama kilikuwa ni kitu cha wazi, unaleta hicho kitu watu wanashauriana. Halafu wanakubaliana. Katiba mpya hii mipango yote ya maendeleo inapangwa na bunge,” alipongeza.

Siku mbili zilizopita, ODM ilitoa barua ikieleza kufukuzwa kwa wabunge wanne na seneta mmoja ambao walikutana na Ruto katika ikulu.

Waliofukuzwa ni pamoja na mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, mbunge wa Suba ya Kusini Caroli Omondi, mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o, mbunge wa Bondo Gideon Ochanda na seneta wa Kisumu Tom Ojienda.