Sifuna afichua kwa nini Passaris hakutimuliwa ODM

Chama hicho kilisema Passaris atalazimika kulipa Sh250,000 kama faini kwa kukaidi chama kando na kuomba msamaha kwa maandishi ndani ya siku saba.

Muhtasari
  • Siku ya Jumanne, Sifuna alisema kuwa Passaris alinyenyekea na kuomba msamaha alipofika mbele ya kamati ya nidhamu kuonesha sababu.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Image: Facebook

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amefichua sababu ya chama cha ODM kuchagua kumwepusha Mwakilishi wa kike wa Nairobi Esther Passaris shoka la kufurushwa ODM.

Siku ya Jumanne, Sifuna alisema kuwa Passaris alinyenyekea na kuomba msamaha alipofika mbele ya kamati ya nidhamu kuonyesha sababu.

"Passaris alikuja na kuomba radhi, hata hivyo, wabunge wengine walidharau wito kuhudhuria kikao cha nidhamu, mwingine alikuja na wakili wa UDA huku mwingine akishindwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu," alisema.

Seneta huyo alibainisha kuwa wabunge hao wengine wa ODM walionyesha madharau ya wazi kwa chama hicho jambo ambalo lilichafua sura ya ODM na hivyo kutimuliwa.

Wiki iliyopita, chama cha ODM kilimtoza faini Passaris kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama  kwa kupigia kura Mswada wa Fedha wa 2023, ambao sasa ni Sheria.

Chama hicho kilisema Passaris atalazimika kulipa Shilingi 250,000 kama faini kwa kukaidi chama kando na kuomba msamaha kwa maandishi ndani ya siku saba.

ODM ilisema azimio hilo lilifikiwa wakati wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama hicho iliyofanyika Jumatano chini ya uongozi wa kiongozi wa Chama Raila Odinga.

"Kwamba Esther Passaris, Mbunge wa Kike katika Kaunti ya Nairobi akaripiwe kwa kukaidi moja kwa moja msimamo wa chama kuhusu Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 na kwamba anapaswa kuomba radhi kwa maandishi ndani ya siku saba," chama hicho kilisema.