Rachel Ruto aandaa tafrija ya dinner kusherehekea mwaka 1 wa Kenya Kwanza

Septemba 13 mwaka jana ndio siku ambayo rais Ruto alikula kiapo akiwa ameshikiwa Biblia na Mama Rachel Ruto walipokuwa wakiapishwa.

Muhtasari

• Hafla hiyo iliandaliwa katika bustani ndogo ya uwanja wa Uhuru Nairobi na ilihudhuriwa na watu wachache.

Mama Rachel Ruto
Mama Rachel Ruto
Image: X

Mama wa taifa Bi Rachel Ruto Septemba 13 aliandaa tafrija ya chakula cha jioni ili kuadhimisha na kusherehekea mwaka mmoja tangu serikali ya Rais Ruto ilipoapishwa na kuchukua hatamu za awamu ya tano.

Hafla hiyo iliandaliwa katika bustani ndogo ya uwanja wa Uhuru Nairobi na ilihudhuriwa na watu wachache.

Mama wa taifa alikiri kwamba mwaka mmoja wa uongozi wa mume wake, Rais Ruto ulikuwa na changamoto si haba lakini siku zote waliweka nguvu na uwepo wa Mungu mbele.

“Tulikusanyika usiku wa leo katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi ili kutoa shukrani kwa baraka ambazo Bwana ametupa katika mwaka huu wa kwanza wa utawala huu. Mwaka uliopita umekuwa wa changamoto, lakini Mungu ametuangalia,” Rachel Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, awali ukijulikana kama Twitter.

Rachel Ruto ambaye amesherehekewa pakubwa kwa kuonesha ulokole wake hadharani na kujijengea sifa na taswira ya mtu ambaye ni muombaji sana na mchamungu aliendeleza wimbi hilo kwa kumshukuru Mungu kwa kuwavusha huku pia akimkabidhi usukani katika kipindi cha miaka minne iliyosalia kuelekea uchaguzi mkuu mwingine.

“Tunamshukuru sana Mungu Mkuu kwa yale aliyoyafanya; hakika ni ya ajabu machoni petu. Kama watu, tunachagua kuhesabiwa pamoja na ‘mkoma’ mmoja aliyerudi kwa Yesu kusema asante. ( Luka 17:15 ) Tunamshukuru Mungu!” alinukuu kifungu cha Biblia.

Aliwahimiza viongozi wote waliochaguliwa kurudi katika ngazi za chini walipo wananchi wapiga kura ili kueneza maendeleo katika njia ya kuboresha maisha ya kila Mkenya.

“Kwa viongozi wote waliochaguliwa, turudi mashinani tuwatumikie wananchi wa Kenya.”