Ruto anapeleka nchi katika mwelekeo ufaao-Wahome Thuku akiri

Aliendelea kusema kuwa anajua watu wengi hawawezi kuamini kuwa anaweza kusema maneno kama hayo

Muhtasari
  • Kupitia akaunti yake rasmi ya Facebook, Wahome Thuku alikiri kwamba anadhani Rais William Ruto anaipeleka nchi katika mwelekeo ufaao.
RAIA WILLIAM RUTO WAKATI WA KONGAMANO LA TABIANCHI KICC
Image: TWITTER

Tangu kufanyika kwa hendisheki kati ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga mnamo 2018, mambo hayajawahi kuwa sawa tena kati ya Uhuru na Rais William Ruto.

Viongozi hao wawili wakuu na washirika wao wamekuwa wakirushiana vijembe na maneno makali na mmoja wa washirika wa Uhuru ambaye amekuwa akimsababishia matatizo ya kila aina Ruto ni Wahome Thuku.

Ijapokuwa Wahome Thuku kwa sasa anaunga mkono kambi ya Azimio ya Raila Odinga, amekuwa akiweka wazi kuwa yuko Azimio pekee kwa sababu ya Uhuru na hivyo basi, amekuwa akielekeza bunduki yake kwa serikali ya Rais William Ruto lakini leo amewashangaza Wakenya baada ya matamshi yake ya hivi punde.

Kupitia akaunti yake rasmi ya Facebook, Wahome Thuku alikiri kwamba anadhani Rais William Ruto anaipeleka nchi katika mwelekeo ufaao.

Aliendelea kusema kuwa anajua watu wengi hawawezi kuamini kuwa anaweza kusema maneno kama hayo lakini kulingana na takwimu zake za mfumuko wa bei, Ruto yuko kwenye njia sahihi.

"HABARI ZA ASUBUHI Watu kadhaa wameniuliza swali hili, "Wahome unafikiri tunaelekea wapi?" Na nimewajibu kwa njia nyingi kama nilivyoweka kwenye Kameme FM Jumatano. Wacha niwe mkweli jinsi ninavyowajibu, nadhani William anatupeleka mahali fulani. Ndio na mimi sio mbishi. Nina hakika huwezi kuamini kuwa ni mimi nikisema hivi kwa hivyo ninatarajia maoni ya "umenunuliwa" kwa wingi, lakini takwimu ziko hapa. MFUMUKO wa bei umepungua kwa miezi kadhaa. Mwisho wa Mei 2023 ilikuwa 8.03%. Mwisho wa Juni 7.88% Mwisho wa 7.28% Mwisho wa 6.73%,"Thuku alisema.