Polisi mstaafu ajijengea kaburi la thamani milioni 7 na kujinunulia jeneza la milioni 3

“Mimi kazi hii nimeifanya nikiwa na akili timamu lakini pia nikaona kwa sababu nina nguvu sasa na uwezo kidogo ninao, nifanye haya mambo kwa kuepuka hadha zile ambazo niliziona mwaka wa 1995 wazazi wangu walipotangulia mbele ya haki." alisema.

Muhtasari

• Alifichua kwamba wala hajachizi lakini ni kujipangia kesho yake kama njia moja aliyoitaja kuwa ni kuepuka matukio aliyoyaona katika misiba ya wazazi.

Mzee aliyejinunulia jeneza na kujijengea kaburi
Mzee aliyejinunulia jeneza na kujijengea kaburi
Image: Screengrab

Afisa mmoja wa polisi ambaye ni mstaafu amegonga vichwa vya habari na kuwashangaza wengi baada ya kujijengea kaburi la kifahari na kujinunulia jeneza ghali akisema ni njia moja ya kujiandaa kwa ajili ya kifo chake.

Tukio hili la ajabu limetokea katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo mzee huyo kwa jina Sabasita amabye ni afisa polisi mstaafu amechukua muda wa miaka 2 kujijengea kaburi lake kwa ukamilifu.

Mzee Sabasita alichimba kaburi hilo pembezoni mwa boma lake lililozingirwa na ua la mawe na mandhari ya maeneo hayo yamepambwa kwa picha mbali mbali zikiwemo picha zake akiwa ndani ya mawanda ya jeshi, picha za marais wa Tanzania miongoni mwa picha zingine ambazo zimezunguka eneo la kaburi.

Katika ukuta mmoja pia amebandika bango ambalo linaonesha vyeo ambavyo amevihudumu akiwa kama mtumishi wa umma – polisi.

Lakini je, mzee huyo askari mstaafu mbona aliamua kujijengea kaburi hali ya kuwa yuko hai? Ni utaahira?

Alifichua kwamba wala hajachizi lakini ni kujipangia kesho yake kama njia moja aliyoitaja kuwa ni kuepuka matukio aliyoyaona katika misiba ya wazazi wake ambao walifariki na kuzikwa kwa taabu.

“Mimi kazi hii nimeifanya nikiwa na akili timamu lakini pia nikaona kwa sababu nina nguvu sasa na uwezo kidogo ninao, nifanye haya mambo kwa kuepuka hadha zile ambazo niliziona mwaka wa 1995 wazazi wangu walipotangulia mbele ya haki, lakini pia kupunguzia gharama familia yangu na pia kuona mbali na gharama, watu wajue kabisa kwamba tunakoelekea ni kifo, kila siku umri unavyoongezeka kwa siku moja pia ule wa kuishi unapungua kwa siku moja,” Mzee Sabasita alisema.

Mzee huyo alifichua kwamba mpaka kufikia hatua za mwisho kabisa, kaburi limechukua karibia shilingi milioni 7 za Kitanzania na pia akasema kuwa maandalizi ya jeneza yako katika hatua za mwisho.

“Sasa hivi kaburi limechukua shilingi milioni 7 lakini pia niko mbioni kuhakikisha kabisa jeneza langu limekwisha kutengenezwa. Nalo litakapokuwa limekamilika ni shilingi milioni 3,” alisema.

Mzee Sabasita alisema kwamba kando na kaburi na jeneza, hakuna kitu kingine ambacho amekiandaa kwa ajili ya mwisho wake duniani, lakini akafichua kwamba wosia wake ndio unaendelea kuandaliwa na mawakili.