Nakuru: Wafugaji walalamika nyani kuvamia ng'ombe malishoni na kunyonya maziwa

Wakulima walisema wamekuwa wakipata hasara kubwakwani wanatumia gharama nyingi kuwalisha mifugo wao lakini jasho lao linaishia vinywani mwa nyani tu.

Muhtasari

• Taarifa hiyo pia ilisema kando na nyani, kero lingine linatokana na wezi ambao wamekuwa na hulka ya kuruka uzio wa maboma kwa lengo la kukama ng’ombe kinyemela.

Ng'ombe wa maziwa
Ng'ombe wa maziwa
Image: BBC NEWS

Wakulima wa ufugaji ng’ombe wa maziwa katika kaunti ya Nakuru wametoa malalamishi yao kwa shirka la huduma za wanyamapori kwa kile walisema ni kero la nyani kuvizia ng’ombe wakiwa malishoni kisha kunyonya maziwa yote.

Kwa mujibu wa taarifa katika gazeti la Taifa Leo, wakulima hao waliteta vikali wakitaka KWS kuhakikisha wameondoa nyani hao ambao sasa wamewapa hasara kwani wanatumia hela nyingi kuwekeza katika chakula na virutibishi vingine vya kuongeza maziwa kwa ng’ombe lakini jasho lao linaishia midomoni mwa nyani.

Taarifa hiyo pia ilisema kando na nyani, kero lingine linatokana na wezi ambao wamekuwa na hulka ya kuruka uzio wa maboma kwa lengo la kukama ng’ombe kinyemela.

“Changamoto kubwa inayowakumba wakulima wadogo hapa ni; hawana uwezo kuajiri vibarua kuwalindia mifugo nyakati za mchana, hivyo basi huwaacha mifugo wao wakizurura.” Mkulima mmoja alinukuliwa na Taifa Leo Digital.

Irene Wambere mfugaji wa ng’ombe na kondoo kutoka eneo la Mzee Wanyama, anasema nyani ni wanyama werevu sana kiasi kwamba wamejifunza kuishi vizuri na mifugo hasa ng’ombe na mbuzi.

“Ndio sababu wengi wetu tuliacha kukama maziwa kitambo kwa sababu siku ikiwa nzuri mfugaji anaweza kupokea labda vikombe viwili tu vya maziwa kwa siku,” alisema.

Edwin Warui, ni mfugaji mwingine Pipeline ambaye ng’ombe wake wa maziwa hawampi faida kamwe kufuatia kero ya nyani.

“Inaonekana ninafugia ng’ombe wangu nyani. Kazi yao imekuwa kuwanyonya wakiwa malishoni,” Bw Warui akaambia Taifa Leo Dijitali.

Hata hivyo, malalamishi yao yamekuwa yakigonga mwamba jambo linalowalazimu kutafuta njia mbadala ya kujilinda dhidi ya hasara za mara kwa mara.

Nyani hao waliarifiwa kutoroka kutoka mbuga ya wanyama ya ziwa Nakuru na kuingia katika maboma kwa lengo la kukata kiu kwa maziwa ya ng’ombe.