Wasioamini Mungu wamtaka binti wa rais Charlene Ruto kuhudhuria mkutano wao

“Tunafahamu kwamba Charlene Ruto ni Mkristo lakini pia tunatambua kwamba Yesu Kristo aliwapenda watu ambao hawakuwa wanamuamini yeye wala babake…." sehemu ya barua ilisoma.

Muhtasari

• Charlene Ruto wiki jana aliteuliwa kama balozi wa kutoa hamasa kuhusu kuchangia damu na wizara ya afya kupitia kwa waziri Susan Nakhumincha.

• Hata hivyo, inasubiriwa kuonwa iwapo binti wa rais atakubali wito huo ikizingatiwa kwamba amekulia katika mazingira ya wazazi walokole.

Charlene Ruto
Charlene Ruto
Image: Facebook

Muungano wa wasioamini katika uwepo wa Mungu nchini Kenya umetoa ombi rasmi kwa binti wa kwanza wa taifa, Charlene Ruto kuhudhuria katika mkutano wao wa kila mwezi mnamo Februari 10.

Katika barua iliyochapishwa kwenye ukurasa wao rasmi wa X, wasioamini Mungu walimuomba binti Ruto kutokosa mkutano huo, na hata kwenda mbele na kumpa maelekezo kamili ya utakakofanyikia.

Charlene Ruto wiki jana aliteuliwa kama balozi wa kutoa hamasa kuhusu kuchangia damu na wizara ya afya kupitia kwa waziri Susan Nakhumincha.

Wasioamini Mungu walisema kwamba lengo lao kuu kumtaka Charlene Ruto kuwepo katka mkutano wao ni kumshawishi kukubali kwambasio kila mtu aliyezaliwa katika dunia hii alizaliwa kwa dhambi.

“Tungependa kumwalika hadharani balozi wa damu wa Kenya, Bi. Charlene Ruto kwa hafla yetu ya kila mwezi, Godless Kona, Jumamosi, tarehe 10 Februari, 2024 katika Hoteli ya Swiss Bennin. Tunatumai kumshawishi Charlene Ruto kwamba kila mtu aliyezaliwa katika sayari hii hajazaliwa katika dhambi,” walisema.

Mkutano wao unaojulikana kama ‘Godless Corner’ ni mkutano unaofanyika kila mwezi ambao unanuia kuwaunganisha wasioamini Mungu kwa fursa za kazi nchini Kenya, walisema katika sehemu ya barua yao kwa binti Ruto.

“Tunafahamu kwamba Charlene Ruto ni Mkristo lakini pia tunatambua kwamba Yesu Kristo aliwapenda watu ambao hawakuwa wanamuamini yeye wala babake…. Tunamchukulia Charlene Ruto kama mtu ambaye ana mawazo wazi na tunatumai atakubali huu wito,” barua hiyo ilisema.

Hata hivyo, inasubiriwa kuonwa iwapo binti wa rais atakubali wito huo ikizingatiwa kwamba amekulia katika mazingira ya wazazi walokole.

Rais Ruto amekuwa akidhihirisha kwamba tangu enzi akiwa mwanafunzi chuo kikuu alikuwa mlokole wa kulihubiri neno na mpaka wakati mmoja kuwa mwenyekiti wa chama cha wakristo chuoni.