Padre wa Katoliki, mganga na baba wakamatwa kwa kumchinja mtoto albino

Kasisi huyo anadaiwa kumshawishi baba mtoto huyo wa miaka 2½ kuanza biashara ya kuuza viungo vya watu albino – akianza na mtoto wake – akisema viungo vyao vina utajiri mkubwa na hata kumtafuta mganga kwa shughuli ya uchinjaji.

Muhtasari

• Polisi walitoa onyo kali kwa makundi ya watu wanaoendekeza Imani za kishirikina ikiwemo kupiga ramli chonganishi kuaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa kuuza viungo vya watu .

Picha ya mtoto Asimwe Novat
Picha ya mtoto Asimwe Novat

Padre ambaye ni mkuu wa Parokea ya kanisa katoliki ni mmoja miongoni mwa watu waliokamatwa kwa tuhuma za kuchinja mtoto mwenye ulemavu wa ngozi kwa nia ya kuuza viungo vya mwili wake.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea wiki iliyopita wilayani Mleba katika mkoa wa Kagera nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa, Baba Paroko, mganga wa jadi na baba mtoto huyo binti mdogo kwa jina Asimwe Novat walikamatwa wakiwa na viungo vya mwili wa mtoto huyo wakiwa wamevifungasha kwenye mifuko ya plastiki wakitafuta mteja wa kununua.

Msemaji wa polisi David Misime alitoa wito kwa watu kuacha tamaduni za jadi zisizo na maziko ambapo baadhi ya watu wanaamini kwamba viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni dawa na utajiri.

Mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 2 na nusu ambaye ni albino alitoweka kutoka nyumbani mwishoni mwa mwezi uliopita na wiki mbili baadae alipatikana akiwa ameuawa kikatili, akiwa amekatwa baadhi ya viungo vyake na mwili wake kufungwa kwenye mfuko wa plastiki na kutupwa kwenye bomba la kupitisha maji barabarani.

“Polisi walianzisha uchunguzi kuanzia Mei 30 hadi kufikia Juni 19 ambapo tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 9 wakiwa na viungo vinavyodhaniwa kuwa ni vya mtoto Asimwe Novat ndani ya mfuko wa plastiki wakitafuta mteja.”

“Watuhumiwa waliokamatwa, ambao walieleza jinsi walivyoshiriki katika tukio hilo, ni pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo, mganga wa jadi na paroko msaidizi wa parokia ya Bugandika ambaye anadaiwa kumtafuta baba mzazi na kumshawishi wafanye biashara ya viungo vya binadamu,” sehemu ya taarifa ya polisi ilisoma.

Paroko huyo pia anadaiwa kuwa yeye ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zake zote.

Polisi walitoa onyo kali kwa makundi ya watu wanaoendekeza Imani za kishirikina ikiwemo kupiga ramli chonganishi kuaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa kuuza viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi waache tabia hiyo.