Seneta amshauri Ruto kuingia TikTok Live kama anataka kufanikisha mazungumzo na Gen Z

Seneta huyo amemshauri rais iwapo angependa kufanikisha mazungumzo yake na vijana wa Gen Z ambao siku za hivi karibuni wameibua masuala kadhaa wakionyesha kutoridhishwa na uongozi wake, basi atenge muda na kuingia TikTok Live.

Muhtasari

• Seneta huyo alisema kuwa TikTok Live ndio njia pekee na sahihi ya kuwapata vijana wote na kusikiliza matakwa yao.

Karungo wa Thang'wa amshauri Ruto kuhusu mazungumzo na Gen Z
Karungo wa Thang'wa amshauri Ruto kuhusu mazungumzo na Gen Z

Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa ameibuka na ushauri kwa rais William Ruto kama njia moja ya kumrahisishia mazungumzo na vijana wa Gen Z.

Seneta huyo amemshauri rais iwapo angependa kufanikisha mazungumzo yake na vijana wa Gen Z ambao siku za hivi karibuni wameibua masuala kadhaa wakionyesha kutoridhishwa na uongozi wake, basi atenge muda na kuingia TikTok Live.

Seneta huyo alisema kuwa TikTok Live ndio njia pekee na sahihi ya kuwapata vijana wote na kusikiliza matakwa yao.

“Riggy G ukitaka kuongea na Gen Z, na pia rais afanye hivyo, wewe ingia tiktok, uende Live, si mambo ndio hayo? Ingia TikTok Live siku moja, useme Gen Z wote kujeni tuongee, watakuongelesha, watakuambia kila kitu na watakuambia mahali wanataka kuenda,” Thang’wa alishauri rais na naibu wake.

Seneta huyo wa UDA pia alimuomba rais Ruto kumpa sikio la usikivu naibu wake kama vile amefanya kuwasikiliza vijana wa Gen Z.

“Mimi nataka kumuomba rais, sababu rais na naibu wake sisi tunawaunga mkono, vile alisikiliza Gen Z, asikilize Riggy G,” alisema.

Ushauri huu unakuja saa chache baada ya mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei kutoa tarifa kwamba rais Ruto ameanzisha timu ya kufanya mazungumzo ya watu kutoka vitengo na matabaka mbalimbali.

Katika barua hiyo kwa vyombo vya habari, makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana waliombwa kupendekeza majina ya watu wawili ambao watajiunga katika timu hiyo ya mazungumzo kueleza matakwa yao.

Koskei alisema kila kundi lina hadi Julai 7 kutoa majina ya wawakilishi wawili wa jinsia yoyote.

Katika siku za hivi karibuni, rais Ruto amejipata chini ya shinikizo kali kutoka kwa vijana ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa uongozi usiowajali.

Licha ya kuitisha mazungumzo na vijana, wengi wanasubiri kuona wawakilishi watatoea wapi, ikizingatiwa kwamba vijana hao wamekuwa wakisisitiza kutokuwa na uongozi maalum.