Mishahara ya wafanyikazi wa mochari unafaa pia uongezwe kwa mara mbili – MP Babu Owino

“Walimu na Madaktari zaidi wanapaswa kuajiriwa. Ada ya vyuo vikuu ipunguzwe kwa 80% na shule ya upili ifanywe bure. Hadi wakati huo, tutakuwa wakaidi,” Babu Owino aliongeza.

Muhtasari

• “Mishahara ya Walimu, Wahadhiri, Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara na wahudumu wa mochari iongezwe ikiwa haitaongezwa mara mbili na Serikali,” Babu Owino alisema.

Babu Owino
Image: maktaba

Siku chache baada ya SRC kuonyesha nia ya kuanza kuwaongezea mishahara na marupurupu maafisa wa serikali, haswa wanasiasa, mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ametoa pendekezo la nyongeza hiyo kutekelezwa pia kwa watoa huduma za muhimu humu nchini.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Owino alipendekeza kwamba iwapo wanasiasa wataongezewa mishahara, pia nyongeza hiyo inafaa itekelezwe mara mbili zaidi kwa madaktari, wahudumu wa mochari, wahadhiri, wauguzi, walimu na hata wataalamu wa maabara.

“Mishahara ya Walimu, Wahadhiri, Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara na wahudumu wa mochari iongezwe ikiwa haitaongezwa mara mbili na Serikali,” Babu Owino alisema.

Katika pendekezo lake, Owino alisema kuwa ikiwa serikali ina nia njema kwa uendelevu wa taifa hili, inafaa kuwaajiri madaktari na waalimu wengi lakini pia kupunguza karo ya vyuo vikuu kwa asilimia 80 na elimu ya shule za upili kuwa bila malipo.

“Walimu na Madaktari zaidi wanapaswa kuajiriwa. Ada ya vyuo vikuu ipunguzwe kwa 80% na shule ya upili ifanywe bure. Hadi wakati huo, tutakuwa wakaidi,” alisema.

Hata hivyo, saa kadhaa baadae, SRC ilitoa taarifa kwamba imefikia uamuzi wa kubatilisha nyongeza ya mishahara baada ya mashauriano ya kina na umma.

SRC ilikuwa imeweka kwenye notisi ya Agosti mwaka jana katika gazeti la Serikali kwamba kungekuwa na nyongeza ya mishahara kwa wanasiasa na maafisa wa serikali kuanzia Julai mosi ambayo ingefaa kuanza kutekelezwa wiki hii.