Binti yangu Gen Z alichangia Sh10k kwa waandamanaji waliojeruhiwa na waliouawa - Sudi

Sudi alifichua kuwa watoto wake vijana walishiriki maandamano hayo yaliyofanyika kwa takriban wiki tatu.

Muhtasari

•Sudi amefunguka kuhusu kuhusika kwa watoto wake katika maandamano yaliyotokea hivi majuzi nchini Kenya yakiongozwa na vijana.

•Mbunge huyo wa chama cha UDA kwa kejeli alidai kuwa Gen Z ni wakaidi lakini akabainisha kuwa watasikilizwa.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Mbunge Oscar Sudi Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Mbunge wa eneo la Kapseret Oscar Sudi amefunguka kuhusu kuhusika kwa watoto wake katika maandamano yaliyotokea hivi majuzi nchini Kenya yakiongozwa na vijana.

Akizungumza wakati wa hafla ya mazishi katika eneo la Kesses, kaunti ya Uasin Gishu mnamo Ijumaa, mwandani huyo wa Rais William Ruto alifichua kuwa watoto wake wenye umri wa ujana walishiriki maandamano hayo yaliyofanyika kwa takriban wiki tatu.

Alizungumza kuhusu bintiye ambaye alimweleza kuhusu maandamano hayo na hata kutuma mchango wa kuwasaidia waathiriwa wa maandamano hayo.

“Hawa watoto wangu Gen Z walikuwa wanakula chakula cha mchana alafu wanaenda maandamano. Kwanza kuna msichana wangu hapa aliniambia ‘Baba hii Gen Z sisi tulikuwa tunafanya mambo yetu mazuri lakini hawa watu wamebadilisha hii kitu wamekuja kutungilia. Lakini hata hivyo, nimetuma shilingi elfu kumi.’

 Nikamuuliza ametuma elfu kumi ya nini? Akaniambia ni ya wale wameumia na wale walikufa. Unaweza kufikiria hata binti yangu mwenyewe alituma pesa,” Sudi alisema.

Mbunge huyo wa chama tawala cha UDA kwa kejeli alidai kuwa Gen Z ni wakaidi lakini akabainisha kuwa watasikilizwa.

Hata hivyo aliwataka kuwa na heshima kwa nchi na wazazi wao hata wanaposhinikiza mabadiliko nchini.

“Mimi nataka niwaencourage Gen Z waheshimu wazazi, tafuta namna ya maisha, utukosoe kwa haki. Tutawaskiza, tutaenda vizuri kama nchi. Lakini usiharibu kilichopo kwa sababu unataka kitu kipya ambacho hujui kinatoka wapi na kinaanza wapi. Mambo ni kuongea na kutafuta njia ya kutengeneza maneno,” alisema.

Sudi alibainisha kuwa yeye binafsi ametoka mbali sana akidai kuwa alianza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 14.