“Ilikuwa wazi kwamba siku moja watu wataanza kuuliza serikali maswali magumu!” – MP Jalang’o

“Kusema ukweli hili lilikuwa limenukia, si tu kwamba ni lini ila ilikuwa wazi kwamba siku moja watu wataanza kuuliza maswali magumu. Tuko na vijana wengi hapa nje ambao wanahisi kwamba hakuna mtu anayewasikiliza.”

Muhtasari

• Mbunge huyo hata hivyo alimtetea rais Ruto kwamba amefanya kadri ya uwezo wake kuwasikiliza vijana na matakwa yao na hata kutekeleza baadhi yayo.

JALANG'O.
JALANG'O.
Image: HISANI

Mbunge wa Lang’ata, Jalang’o amekiri kwamba vuguvugu la kuiwajibisha serikali kutoka kwa vijana wa Gen Z ambalo linaendelea humu nchini kwa mwezi sasa ni suala ambalo muda wake ulikuwa umefika.

Akizungumza kwenye runinga ya TV47, Jalang’o alisema kwamba kutoka siku za nyumba, alikuwa na hisia kwamba ingefika siku ambapo vijana watachoka na kuanza kuiwajibisha serikali kwa kuiuliza maswali magumu.

Mbunge huyo ambaye kabla ya kujitosa kwenye siasa alikuwa mtangazaji na mchekeshaji alisema kwamba hilo lilikuwa wazi kwa kuwa Kenya ya sasa ina vijana wengi ambao wamesoma pasi na kuwa na ajira na ambao wamefunguka akili.

“Kusema ukweli hili lilikuwa limenukia, si tu kwamba ni lini ila ilikuwa wazi kwamba siku moja watu wataanza kuuliza maswali magumu. Tuko na vijana wengi hapa nje ambao wanahisi kwamba hakuna mtu anayewasikiliza.”

“Na kwa muda mrefu walikuwa wanahisi kwamba hakuna mtu alikuwa anawapa sikio, na tabaka la wanasiasa lilikuwa ni tabaka lililojitenga kivyake, ambao walifikiria kwamba wana uamuzi kaitka kila kitu wanachotaka, lakini sasa wakati suala hili lilichemka kufikia kiwango cha kutoweza kuzuilika, walijitokeza. Na sasa hakuna njia nyingine, ni ima uwasikilize au uondoke ofisini,” Jalang’o alisema.

Mbunge huyo hata hivyo alimtetea rais Ruto kwamba amefanya kadri ya uwezo wake kuwasikiliza vijana na matakwa yao na hata kutekeleza baadhi yayo.

“Siku baada ya nyingine, hasira zinapungua kwa sababu rais anawasikiliza. Hasira haziko jinsi zilivyouwa mwanzo. Huku rais akiwasikiliza na vitu vikianza kubadilika juu chini, mswada wa fedha ushatupwa nje, mawaziri wote walikuwa wametumwa nyumbani, pengine wakati Gen Z watajitokeza kuandamana tena watasikilizwa zaidi na zaidi na najua siku moja tutafikia kiwango cha usawa ambapo kila mmoja atakuwa na furaha na tutasonga mbele,” alisema.