Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amedai kwamba amepokea mwaliko kutoka kwa idara ya Ujasusi, DCI katika kile alidai kwamba wamemuomba kuwapa usaidizi katika kujichunguza mwenyewe.
Kupitia kwa kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Owino alichapisha barua ya mwaliko kutoka kwa DCI akisema kwamba ametakiwa kesho Jumatano kujitokeza mbele yao ili kuwapa msaada huo wa ‘kujichunguza’.
“Nimepokea barua ya mwaliko kutoka kwa DCI wananitaka niwasaidie kujichunguza mwenyewe, huu ni wazimu kabisa,” Babu Owino alinukuu picha ya barua hiyo.
Katika barua hiyo, Babu Owino alitakiwa kujiwasilisha ili kutoa maelezo ya kile anadaiwa kuwa ni mmoja kati ya wahusika wa utakatishaji wa fedha na uchochezi.
“Ninachunguza kuhusu kudaiwa kuchochea na kujihusisha katika utakatishaji fedha ambapo naamini wewe Babu Owino umehusika ama unaweza kuwa na taarifa ambazo zitasaidia katika uchunguzi wa kesi hizi. Hivyo kulingana na uwezo niliopewa ninakuomba ujiwasilishe katika kituo cha DCI, Nairobi Julai 24 majira ya saa tatu asubuhi ili kuwasilisha taarifa zote ulizo nazo kuhusu kesi hii,” sehemu ya barua hiyo kutoka kwa afisa wa DCI inasomeka kwa sehemu.
Owino amekuwa si mgeni katika kamata-kamata za polisi tangu alipoingia kwenye siasa takribani miaka 7 iliyopita.