Mwendesha pikipiki aliyeanguka na kumwaga maziwa barabarani afarijiwa kwa njia ya kipekee

"Tunamuelewa. Tunasikia maumivu yake. Tunasema pole kwa kumzawadia siku 3 za likizo yenye malipo kamili hadi Mombasa!,” Expeditions walisema.

Muhtasari

•Kampuni ya Expeditions Maasai Safaris ilibainisha kuwa bidii na ukakamavu wake zinastahili yeye kupata mapumziko.

•Kampuni hiyo ilibainisha mara zingine watu huwa na siku mbaya kwenye kazi zao na walisema kwamba walihisi maumivu yake.

amezawadiwa kwa safari ya siku 3, Mombasa.
John Kinyua kutoka Embu amezawadiwa kwa safari ya siku 3, Mombasa.
Image: EXPEDITIONS MASAAI SAFARIS

Siku chache tu baada ya kukumbwa na huzuni baada ya maziwa aliyokuwa akisafirisha kwenye pikipiki yake kumwagika kwenye barabara mbovu katika Kaunti ya Embu, John Gitonga Kinyua sasa amefarijiwa kwa safari ya Pwani na moja ya kampuni kubwa za utalii nchini Kenya.

Mwendesha pikipiki huyo ambaye hivi majuzi alivutia sana hisia za Wakenya baada ya picha za maziwa yaliyomwagika kuvuma kwenye mitandao ya kijamii, alijawa na tabasamu kubwa usoni mwake siku ya Jumanne wakati akipokea vocha ya zawadi ya safari ya siku tatu ya Mombasa iliyolipiwa kikamilifu.

Kampuni ya Expeditions Maasai Safaris ilibainisha kuwa bidii na ukakamavu wake zinastahili yeye kupata mapumziko, hivyo sababu yao ya kumpa zawadi hiyo.

"Kutoka kwa maziwa yaliyomwagika hadi ufuo wa jua, bidii ya John Gatia inastahili mapumziko. Furahia likizo yako mjini Mombasa kama zawadi ya kujitolea na ukakamavu wako,” Expeditions Maasai Safaris ilisema Jumanne jioni.

Kampuni hiyo ilijitosa katika kumtafuta kijana huyo kutoka kaunti ya Embu baada ya picha za masaibu yaliyompata kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yao, Expeditions ilibainisha kuwa mara zingine watu huwa na siku mbaya kwenye kazi zao na walisema kwamba walihisi maumivu yake.

“Tunamtafuta! Wanaume hupitia mengi katika kutafuta maisha bora.  Sote tuna siku njema na mbaya ofisini. Huu ni mfano wa siku mbaya. Tunamuelewa. Tunasikia maumivu yake. Tunasema pole kwa kumzawadia siku 3 za likizo yenye malipo kamili hadi Mombasa!,” kampuni hiyo ya utalii ilisema mapema wiki hii.

Siku chache zilizopita, mwanaume huyo alikuwa akipitia barabara yenye matope inayoteleza katika kaunti ya Embu wakati pikipiki yake ilipopoteza mwendo na kupinduka na kusababisha shehena ya maziwa yake kumwagika barabarani.

Picha za tukio hilo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mkubwa na hisia mseto kutoka kwa Wakenya wengi.