• Alisema kwamba wanasiasa wengi wameshindwa kutimiza lengo la ugatuzi ambalo lilikuwa ni kuleta huduma karibu na mwananchi
Mwanaharakati Eric Omondi ametishia kuanzisha mchakato wa kukusanya kura ya maoni kutoka kwa wakenya kwa lengo la kufanyia marekebisho baadhi ya nyadhifa ya kisiasa.
Akizungumza kaitka kituo kimoja cha habari humu nchini siku ya Ijumaa, Omondi alisema kwamba Wakenya wamewakilishwa kupita kiasi na hivyo kuna haja ya kupunguza au kufutilia mbali baadhi ya nyadhifa za kisiasa.
Mwanaharakati huyo alisema kuwa baadhi ya mageuzi ambayo watalenga ni kupunguzwa kwa kaunti kutoka 47 hadi 8, kufutiliwa mbali kwa nyadhifa za maseneta na wawakilishi wa kike miongoni mwa mageuzi mengine.
“Tunaenda kuanzisha mchakato wa kukusanya kura ya maoni, ukiongozwa na Eric Omondi, kuondooa kaunti zote 47 na kuzipunguza hadi 8 kama mikoa zamani. Tunaenda kuondoa kabisa maseneta, wawakilishi wa kike, wabunge maalum, hata hao MCAs wachunge sana juu sijaona kazi yao,” Omondi alisema.
Alisema kwamba wanasiasa wengi wameshindwa kutimiza lengo la ugatuzi ambalo lilikuwa ni kuleta huduma karibu na mwananchi wa kawaida na badala yake walemeta ufisadi kutoka serikali za juu hadi kwa kaunti.
“Lengo lilikuwa kuleta huduma muhimu karibu na mwananchi wa kawaida, lakini hawa wameleta ufisadi. Hakuna kazi MCA wanafanya, wananchi wanachanganyikiwa kwa sababu hawajui ni kiongozi yupi anayefaa kufanya maendeleo yepi. Wakenya wamewakilishwa kupita kiasi, mara rais, mara gavana, seneta, mwakilishi wa kike, mbunge, MCA... wote wanawakilisha aje mtu mmoja?” Omondi alihoji.