•"Tunazunguka nchi nzima kukusanya saini. Tunachohitaji ni saini milioni. Hiyo inapaswa kutuchukua chini ya wiki mbili," Eric amesema.
•Eric alisema mlipa ushuru ameelemewa na kubainisha kuwa nia ya ugatuzi ilikuwa kusambaza huduma lakini nchi ikaishia kusambaza ufisadi.
Mchekeshaji na mwanaharakati maarufu wa Kenya Eric Omondi ameanzisha mchakato wa kukusanya saini ili kuipeleka nchi kwenye kura ya maoni.
Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show anasukuma kupunguzwa kwa idadi ya kaunti na vile vile kuondolewa kwa nafasi ya useneta, nafasi ya mwakilishi wa kike, wabunge walioteuliwa, na MCAs walioteuliwa.
Kulingana naye, Kenya ina uwakilishi mkubwa na kuna haja ya kupunguza watu katika nafasi za uongozi.
“Kenya ina uwakilishi mkubwa. Mtu mmoja anawakilishwa na rais, naibu rais, gavana, naibu gavana, mbunge, seneta, mwakilishi wa kike, MCA, ako na kamishna wa mkoa, kamishna wa kaunti, kamishna msaidizi wa kaunti, chifu, chifu, na mzee wa kijiji. Mkenya mmoja anawakilishwa na watu 16 wanaofanya jambo moja,” Eric alisema wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika Nairobi.
Aliongeza, "Tunazunguka nchi nzima kukusanya saini. Tunachohitaji ni saini milioni. Hiyo inapaswa kutuchukua chini ya wiki mbili."
Mchekeshaji huyo alilinganisha Kenya na Marekani akisema kuwa nchi hiyo ya magharibi yenye raia wengi ina maafisa wachache wa serikali kuliko Kenya.
“Walipa kodi wanabeba mzigo wa kulipia ofisi zinazowiana. Tuko na waziri wa michezo katika serikali ya kitaifa, tuko na waziri wa michezo katika serikali ya kaunti. Tuko na waziri wa mazingira huko juu, tuko na waziri wa mazingira huku chini. Kwani mazingira ni ngapi?” alihoji.
Eric alisema mlipa ushuru ameelemewa na kubainisha kuwa nia ya ugatuzi ilikuwa kusambaza huduma lakini nchi ikaishia kusambaza ufisadi.
Mwanaharakati huyo ambaye amekuwa akiongea sana kuhusu masuala ya kisiasa katika miaka michache iliyopita alitoa kauli hizo wakati wa mkutano na wanahabari aliofanya katika Hoteli ya Serena, Nairobi mnamo Agosti 20.