•Huku akijibu wakili huyo, msemaji Isaac Mwaura alikanusha kufahamu mazungumzo yoyote kati yake na Rais.
•Msemaji wa ikulu Hussein Mohamed pia alikanusha madai ya rais Ruto kumpigia simu Morara na kuyataja kuwa ya uongo.
Siku ya Jumatano jioni, msemaji wa serikali Isaac Mwaura na msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed wote walikanusha waziwazi madai ya wakili na mwanaharakati Morara Kebaso kwamba rais William Ruto alimtafuta kwa ajili ofa ya kazi serikalini.
Morara ambaye katika muda wa wiki kadhaa zilizopita amekuwa akifichua miradi iliyofeli ambayo awali ilizinduliwa na rais alikuwa kwenye runinga ya Citizen Jumatano usiku ambapo alidai kuwa rais alituma wawakilishi wake kuzungumza naye kabla ya kumpigia simu moja kwa moja kuhusu kumpa kazi.
Wakili huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter alisisitiza madai yake akisema kwamba hatazingatia kuthibitisha iwapo simu na rais ilifanyika kweli. Pia aliweka wazi kuwa hana nia ya kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza.
“Sitafuata nyayo za wale viongozi waliokuwa wanamrekodi rais au kumweka kwenye loud speaker ili kuthibitisha hoja. Sidhani kama ni tabia njema. Kwa sababu hiyo, sitazingatia kuthibitisha kama ilifanyika au la,” Morara Kebaso aliandika.
Aliongeza, “Isaac Mwaura anajua ilitokea. William Ruto anajua kilichotokea. Mwisho wa hadithi. Tuzingatie kutengua mahali ametenga. Wito huo hauna umuhimu wowote katika kupigania utawala bora na kukomesha rushwa. Tusigeuze mazungumzo. Taifa linafahamu mwongo ni nani kati yangu na Dkt William Ruto.”
Huku akijibu wakili huyo, msemaji Isaac Mwaura alikanusha kufahamu mazungumzo yoyote kati yake na Rais.
Pia alikana kuwahi kuzungumza na kijana huyo kuhusu ofa ya kazi na akafafanua kuhusu kukutana kwao hivi majuzi.
“Sifahamu wito wowote kutoka kwa Rais kuja kwenu. Tafadhali chunguza dhamiri yako na uonyeshe uzalendo. Nimekutana nawe kwenye KICC kama raia mwenzangu yeyote. Kuwa mkweli kwako mwenyewe,” Mwaura alijibu.
Msemaji wa ikulu Hussein Mohamed, alipopigiwa simu na mwanahabari Jeff Koinange, pia alikanusha madai ya rais Ruto kumpigia simu Morara na kuyataja kuwa ya uongo.
“Ni jambo lisiloaminika tu. Nimeshtushwa na anachosema Morara. Nashangaa kwa nini anadanganya kwenye TV ya taifa kwamba rais alimuita. Simu kama hiyo haijawahi kutokea, ni mawazo yake tu,” Hussein alisema.
Pia alimkosoa Jeff kwa madai ya Morara akisema kwamba mwanahabari huyo alipaswa kudai ushahidi.