Mamake Morara Kebaso afunguka jinsi uanaharakati wa mwanawe umeathiri maisha yake

Alibainisha kuwa amemtoa mwanawe kwa Wakenya na amesalia tu kumuombea na kumtakia heri.

Muhtasari

•Mama mzazi wa Kebaso alichukua fursa kuzungumzia maoni yake kuhusu kazi ambayo mwanawe amekuwa akifanya.

•Pia alifunguka kuhusu jinsi mwanawe huyo amefanya hadhi yake katika jamii kubadilika.

Morara Kebasa na mama yake mzazi
Image: HISANI

Mwanaharakati wa kisiasa David Morara Kebaso hivi majuzi aliandaa hafala ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo jamaa na marafiki zake walialikwa.

Mmoja wa waliokuwepo katika hafla hiyo ni mama yake mzazi ambaye alitumia jukwaa hilo kuzungumzia maoni yake kuhusu kazi ambayo mwanawe amekuwa akifanya.

Katika hotuba yake, mamake Morara alibainisha kuwa uamuzi wa kufuatilia serikali ambao mwanawe alichagua kuchukua haujakuwa rahisi kwake na familia kukabiliana nao.

"Haikuwa jambo rahisi kwangu pia kama mama yake kwa sababu wakati wowote Mercy ,binti yangu, anaponipigia simu, mimi hujiuliza "nini kimetokea?" Mamake Morara alisema.

Hata hivyo, mama huyo alifichua kuwa kila mara amekuwa akiombea ustawi wa mwanawe na akasisitiza kwamba maombi hayo yamempa ujasiri.

“Kama mama aliyemleta hapa duniani, ninasadiki kwamba Mungu ana kusudi kubwa maishani mwake. Ninaamini kwamba ataishi ili kutimiza kusudi ambalo Mungu alimuumba katika dunia hii. Kwa hivyo, nataka kusema maisha juu yake," alisema.

Mamake Morara aliendelea kumuomba mwanawe aweze kujitabiria maisha marefu pia ili aishi kutimiza kusudi ambalo Mungu analo kwake.

Pia alifunguka kuhusu jinsi mwanawe huyo amefanya hadhi yake katika jamii kubadilika.

“Kwa sasa mimi ni mama ya mtu mashuhuri, kwa sababu watu wanakuja kuniuliza kama mimi ndiye mama wa Morara Kebaso. Wengine huniita kisha hunitambulisha kwa watu nisiowafahamu. Ninawaambia, ‘huyo si mtoto wangu, huyo ni mtoto wenu, sasa mnammiliki,” alisema.

Mamake Kebaso alibainisha kuwa amemtoa mwanawe kwa Wakenya na amesalia tu kumuombea na kumtakia heri.