Fahamu kwa nini Gachagua bado hajahamia katika makazi rasmi ya Naibu Rais

Gachagua alisema bado hajakubali ukweli kwamba yeye ndiye naibu rais wa Kenya.

Muhtasari

•Licha ya Rais William Ruto kuhamia ikulu siku hiyohiyo alipoapishwa, Gachagua bado anaishi nyumbani kwake Karen.

•DP alisema nyumba yake ya Karen inasalia kuwa maalum kwa familia yake kutokana na kumbukumbu inayobeba.

Naibu rais mteule Rigathi Gachagua
Naibu rais mteule Rigathi Gachagua
Image: MAKTABA

Rigathi Gachagua bado hajahamia katika makazi rasmi ya naibu rais huko Karen, Nairobi takriban wiki moja baada ya kuapishwa kuingia afisini.

Licha ya Rais William Ruto kuhamia ikulu siku hiyohiyo alipoapishwa, Gachagua bado anaishi nyumbani kwake Karen.

Katika mahojiano na KTN News Jumapili, Gachagua alisema anahitaji muda kutafakari mambo mengi yanayoendelea maishani mwake kabla ya kuhamia humo.

Gachagua alisema bado hajakubali ukweli kwamba yeye ndiye naibu wa Rais wa Kenya.

"Mambo yanayoendelea karibu yangu ni makubwa sana. Bado sijazoea, kutafakari na kukubali hali mpya na hadhi na yote. Ni balaa sana. Nitahitaji kuchukua muda lakini baada ya muda nitafanya kuhamia katika makazi rasmi," alisema.

Aliongeza:

“Bado nipo hapa nikijaribu kutafakari na kwa vyovyote vile, hakuna haraka, kazi inaendelea na kwa muda muafaka, nitahamia kwenye makazi rasmi, lakini nitahitaji kutafakari mabadiliko yote, na mambo yanayonizunguka."

Naibu Rais alibainisha zaidi kwamba nyumba yake ya Karen, hata hivyo, inasalia kuwa maalum kwa familia yake kutokana na kumbukumbu inayobeba.

"Nina uhusiano wa kihisia na nyumba hii, watoto wangu walikulia hapa, wazazi wangu waliishi nami hapa kwa miaka mingi," Gachagua alifichua.

"Inahuzunisha sana kwangu kuenda mbali na nyumba ambayo nimeishi kwa miaka 24.”