Khaminwa afichua kwa nini hamiliki smart phone licha ya kuwa mwanasheria miaka 53

Khaminwa ana vifaa vichache sana vya kielektroniki katika ofisi yake iliyoko Lavington, Nairobi.

Muhtasari

•Wakili Khaminwa alisema kuwa kutomiliki simu ya kisasa ni uamuzi wa kibinafsi alioufanya miaka mingi iliyopita.

•Khaminwa alibainisha kuwa katika miaka ya 80s, serikali ilikuwa ikijaribu kufuatilia mazungumzo ya wanaharakati kupitia simu.

Wakili John Khaminwa
Image: MAKTABA

Mwanasheria Mkongwe wa Kenya hivi majuzi alishiriki mahojiano na Nation Africa ambapo alifunguka kuhusu taaluma yake ya sheria ya zaidi ya miongo mitano na maisha yake ya kibinafsi.

Miongoni mwa mambo ya kibinafsi ambayo alihojiwa ni sababu ya yeye kumiliki simu ya kawaida licha ya kuwa na uwezo wa kununua simu ya kisasa (smartphone).

Khaminwa ambaye amekuwa akitoa huduma za sheria kwa miaka 53 iliyopita alisema kuwa kutomiliki simu ya kisasa ni uamuzi wa kibinafsi alioufanya miaka mingi iliyopita.

"Ni uamuzi wa kibinafsi kwamba niliamua kutomiliki smartphone," Khaminwa aliambia Nation.

Pia alibainisha kuwa hapo nyuma katika miaka ya 80s, serikali ilikuwa ikijaribu kufuatilia mazungumzo ya wanaharakati, sababu nyingine kwa nini inambidi kuwa makini zaidi.

Wakili huyo ambaye amehusika katika kesi nyingi zinazohusu wanasiasa wakuu nchini Kenya ana vifaa vichache sana vya kielektroniki katika ofisi yake iliyoko Lavington, Nairobi.

Khaminwa alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 87 mnamo Septemba 10. Aliingizwa katika ulimwengu wa sheria mwaka 1970 na akaajiriwa kufanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa.

 Anajulikana kuwa tayari kila wakati kujitokeza na kuwakilisha watu wanaomini kuwa haki zao zimekiukwa. Hata hivyo, pia amepatwa na mikasa mikubwa maishani ambayo inamlemea anapoanza kuwaza kuyahusu. Hii ni pamoja na kumpoteza mkewe Joyce Khaminwa takriban miaka tisa iliyopita baada ya kuwa pamoja kwa takriban miongo mitano.

“Namkumbuka sana mke wangu. Alikuwa jaji mahiri,” Khaminwa aliambia The Star akiwa na uso wa huzuni ghafla wakati wa mahojiano yaliyopita.

 Joyce Khaminwa, mke wake wa miaka 48, alifariki mwaka wa 2014 katika Hospitali ya Nairobi. Alikuwa jaji katika Mahakama Kuu.

“Ndiyo, tulikuwa na ndoa nzuri kwa zaidi ya miaka 48. Alikuwa mshirika gani,” alisema.

Khaminwa pia alizungumza na The Star kuhusu kifo cha mtoto wake wa kwanza Albert Khaminwa, aliyefariki mwaka 2017, akimtaja kuwa ndiye aliyetembea katika nyayo zake, na kuwa wakili. Wakati wa kufa kwake, Albert alikuwa mshirika mkuu katika Khaminwa & Khaminwa Advocates, kampuni ya uwakili inayoendeshwa na mwanasheria huyo mkongwe.

"Alikuwa mwana mwenye kipaji," alisema.

Dkt Khaminwa hapo awali amewahi kuwakilisha watu mashuhuri na hodari, huku baadhi ya kesi zikimfanya azozane Rais mstaafu Daniel arap Moi, zikimweka kizuizini.