Miujiza! Rachel Ruto asimulia jinsi alivyoomba hadi maji chafu yakabadilika kuwa safi

Muhtasari

•Rachel alifichua kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakipitisha maji ya kisima kile kwenye mashine za kusafisha.

•Siku mbili tu baada ya maombi yake maji yale yalikuwa yamebadilika na kuwa safi na hata hawalazimiki tena kutumia mashine za kuyasafisha.

Image: FACEBOOK// RACHEL RUTO

Mke wa naibu rais William Ruto, Rachel Ruto amesimulia kuhusu 'muujiza' ambao alifanya hivi majuzi nyumbani kwao katika mtaa wa Karen.

Akihutubia makasisi kutoka makanisa mbalimbali ya Kiinjili wakati wa mkutano wa maombi, Rachel alisimulia jinsi alivyoombea kisima chao ambacho kimekuwa kikitoa maji chafu kwa takriban miongo miwili hadi maji yakaanza kuwa safi.

"Mwaka wa 2003 tulichimbua kisima kwetu nyumbani. Tulipochimbua kisima hicho, maji yalipotolewa ili kuangaliwa  na maabara tuliambiwa hatungeweza kunywa maji yale jinsi yalivyokuwa hadi yasafishwe," Rachel alisimulia.

Rachel alisema baada ya kubainika kuwa maji ya kisima chao yalikuwa chafu mumewe alinunua mashine ghali za kuyasafisha.

Alifichua kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakipitisha maji ya kisima chao kwenye mashine alizonunua Ruto, jambo ambalo limewagharimu pesa nyingi.

"Nimekuwa nikijiuliza, na nikiamua kuenda kuombea maji yale, je kuna uwezekano yatakuwa safi. Hilo ndilo nimeishi kujiuliza. Imekuwa ikifanyika tangu 2003. Hivi majuzi mashine za kusafisha zimekuwa na shida na tulitumia pesa nyingi kununua na niliita timu yangu kutoka Eldoret kututengezea," Alisimulia.

Bi Ruto amesema wiki moja tu baada ya mafundi kutengeneza mashine ziliharibika tena na wakawa hawawezi kusafisha maji.

Hapo ndipo alipoamua kuombea kisima kile na baada ya siku chache tu maombi yake yakawa yamejibiwa.

"Nilienda jikoni, nikachukua bakuli, nikaweka chumvi na kuenda kwenye kisima. Nilienda nikayarudia maneno ya Elisha.Nilisema maji hayo hayatakuwa chafu tena. Niliombea maji ya kisima kile. Kwa kuwa kulikuwa kunataka kunyesha nilikimbia ndani ya  nyumba na nikaendelea na shughuli zangu," Alisimulia Rachel.

Rachel amesema baada ya siku mbili tu maji ya kisima chao yalikuwa yamebadilika na kuwa safi na hata hawalazimiki tena kutumia mashine za kuyasafisha.