Ninaomba kila siku uachilie jamii ya Wakamba kutoka kwa gereza-Kivutha ampasha Kalonzo

Gavana huyo wa zamani alifichua kwamba alikuwa akiomba kwamba Wakamba wasikubali kudanganywa.

Muhtasari
  • Mnamo Jumatatu, Kivutha alimsuta Kalonzo kutokana na matamshi yake ya hivi majuzi ambapo aliwaomba Wakenya wamwombee huku akianza kutangaza azma yake ya urais 2027
Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana
Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana
Image: HISANI

Aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana amemkashifu kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu mipango yake ya kuwania urais katika uchaguzi wa 2027.

Mnamo Jumatatu, Kivutha alimsuta Kalonzo kutokana na matamshi yake ya hivi majuzi ambapo aliwaomba Wakenya wamwombee huku akianza kutangaza azma yake ya urais 2027.

"Nilipitia chaguzi tatu zilizoibwa 2013, 2017 na 2022. Tafadhali niombee nitoke gerezani," Kalonzo alidai hata wakati hakuna ushahidi wa kutosha kwamba kulikuwa na utovu wa nidhamu.

Kulingana na Kivutha, kiongozi huyo wa wiper alikuwa akijiandaa kwa mchezo wa mwisho ambao anajua hautafaulu ili aweze kupata uwekezaji wa kisiasa wa kustaafu.

"Mnajitayarisha kwa MCHEZO wenu wa MWISHO wa azma ya kugombea urais 2027 (mkijua mtafeli) ambapo jamii yenu inawapa magavana/Wabunge/Maseneta/ MCAs waliochaguliwa ili muishie na uwekezaji wa kisiasa wa kustaafu," alisema.

Gavana huyo wa zamani alifichua kwamba alikuwa akiomba kwamba Wakamba wasikubali kudanganywa.

Kivutha aidha alisema anamuombea Kalonzo aachilie jamii ya Wakamba kutoka katika gereza halisi.

“Gereza gani? Ninaomba kila siku kwamba unaweza kuachilia taifa la Kamba kutoka kwa gereza halisi la ukame, njaa ya kudumu, umaskini na ukosefu wa maendeleo,” Kivutha alisema.

"Ninaomba kwamba Kamba wajue umewafunga gerezani kutoka kwa Yatta na Tseikuru," aliongeza.