Njugush na Butita wanatengeneza pesa nyingi kuliko mshahara wangu- rais Ruto akiri

Rais Ruto amewapongeza Njugush na Eddie Butita kwa kuchuma pesa kutumia sanaa zao.

Muhtasari

•Ruto alidokeza kwamba wachekeshaji hao wamefanikiwa kutengeza pesa nyingi kwa kuuza maudhui yao kwenye mitandao ya kidijitali.

•Rais pia alisisitiza kuhusu dhamira yake ya kubadilisha hali ya tasnia ya ubunifu nchini

amewapongeza wachekeshaji Njugush na Butita kwa kutumia mitandao kutengeneza pesa.
Rais William Ruto amewapongeza wachekeshaji Njugush na Butita kwa kutumia mitandao kutengeneza pesa.
Image: HISANI

Rais William Ruto amewapongeza wachekeshaji Timothy Kimani almaarufu Njugush na Eddie Butita kwa kuchuma pesa kutumia sanaa zao.

Akizungumza katika Ikulu siku ya Ijumaa, amri jeshi mkuu alidokeza kwamba wachekeshaji hao mashuhuri wamefanikiwa kutengeza pesa nyingi kwa kuuza maudhui yao kwenye majukwaa ya kidijitali.

"Hao vijana wawili unaowaona hapo wanaingiza pesa nyingi kuliko mshahara wangu. Msiwaone hivi hivi ati wamevaa T-shirt sijui namna gani. Jamaa hawa wawili ni wajasiriamali makini," rais alisema Ijumaa.

Rais aliwapongeza wawili hao kwa kuwaongoza vijana katika kutengeneza pesa kwa kutumia mitandao ya kidijitali kama vile YouTube. Aidha, aliwahimiza vijana wengine wa Kenya kuiga mfano wao na kutumia mitandao ya kidijitali kuchuma pesa.

Ruto alizungumza wakati alipowaalika wabunifu na wahitimu wa tamasha la drama kwa tamasha la Serikali katika ikulu.

Rais pia alisisitiza kuhusu dhamira yake ya kubadilisha hali ya tasnia ya ubunifu nchini. Alisema kuendelea mbele, wabunifu wanapaswa kujua kwamba serikali yake inawachukulia kwa uzito kama msingi mkuu wa uchumi.

Ruto alisema hakuhudhuria Tamasha la Drama mjini Mombasa kwa sababu alitaka wafike Ikulu ya Nairobi kutangaza mwanzo mpya.

"Tunaweza kuongeza kiwango cha juu katika masuala ya sanaa na wabunifu, kilichotokea leo Ikulu hakijawahi kutokea," Rais alisema.

"Nilitaka tuanzie hapo ili muanze kufahamu kwamba wabunifu ni biashara kubwa na kwamba tunaichukulia kama vile serikali ya Kenya."'

Rais alisema kama alivyoahidi, serikali yake itatoa msukumo mpya kwa nafasi inayozunguka michezo, vijana, wabunifu na tasnia nzima ya sanaa.

Alisema tasnia ya ubunifu ni kichocheo muhimu cha kampeni dhidi ya tabia mbaya za kijamii ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.