Rais Ruto hatimaye afunguka kwa nini amepoteza uzito wa mwili

"Niliamua kuikata kwa sababu ile kibarua niko nayo si kidogo, unahitaji kuwa macho sana, ili kufanya kazi vizuri zaidi," alisema.

Muhtasari

•Ruto alifichua kuwa shinikizo lililotokana na kampeni lilimlazimu kuwa na ratiba za ulaji zisizo za kawaida.

•Siku za hivi majuzi, Ruto amejitokeza hadharani akionekana mwepesi kuliko alivyokuwa wakati wa kampeni.

Rais William Ruto
Image: PCS

Hatimaye Rais William Ruto amefichua ni kwa nini amepunguza uzito wa mwili, jambo ambalo limevuta hisia za Wakenya katika siku za hivi majuzi.

Akizungumza wakati wa mahojiano na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi, mkuu wa nchi alifichua kuwa shinikizo lililotokana na kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 lilimlazimu kuwa na ratiba za ulaji zisizo za kawaida.

"Tuliingia kwenye uchaguzi na unajua ukiwa na uchaguzi kunakuwa na presha kubwa, wakati mwingine unatoa presha ya chakula na huna muda wa kwenda kufanya mazoezi. Lazima ufanye hivi na vile na huna muda wa kwenda kufanya mazoezi na wakati mwingine unakula. Kwa sababu hujui ni lini utapata mlo unaofuata, wakati mwingine, unakula kupita kiasi ,” Ruto alisema.

 Aliongeza "Niliamua kuikata kwa sababu ile kibarua niko nayo si kidogo, unahitaji kuwa macho sana, ili kufanya kazi vizuri zaidi.

Ruto alikuwa akijibu swali lililoulizwa na mtangazaji Eric Lattif aliyemuuliza kuhusu mpango wake wa mazoezi.

"Mheshimiwa Rais, unaonekana vizuri, na watu wamekuwa wakitoa maoni yao, wakiuliza ikiwa ni mazoezi au lishe," Eric aliuliza swali.

Rais alifanya kampeni kwa nguvu zote za uchaguzi wake wa urais ambao ulimfanya kushinda uchaguzi huo.

Alisema kipindi cha kampeni kilikuwa kigumu, kwani mtu hata husahau kula.

"Unapoenda kwenye uchaguzi, huna muda wa kufanya mazoezi," Ruto alisema.

Siku za hivi majuzi, Ruto amejitokeza hadharani akionekana mwepesi kuliko alivyokuwa wakati wa kampeni.

Maendeleo hayo mapya yamezua gumzo miongoni mwa Wakenya wakihoji ni kwa nini kuna mabadiliko makubwa kwenye mwili wa rais. Rais hata hivyo sasa ameweza kuweka mambo wazi.