Sababu ya kushangaza kwa nini jamaa alimuua mwanafunzi wa Kisii Polytechnic yafichuliwa

Marehemu Lucy Boke na mshukiwa walikuwa kwenye uhusiano na hata walikuwa na mtoto wa miezi tisa pamoja.

Muhtasari

•Familia ya Lucy Boke imedai mshukiwa alikasirika kwa kuwa hangeweza kumuoa mwanadada huyo kwa vile walikuwa na uhusiano wa kinasaba.

•Mamake marehemu aliviambia vyombo vya habari kuwa bintiye alikataa ombi la mzazi huyo mwenzake la kutaka kuolewa naye.

 

Marehemu Lucy Boke
Image: HISANI

Stephen Orengo, jamaa anayesemekana kumuua mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Kisii National Polytechnic anadaiwa kuchukua hatua hiyo ya kusikitisha baada ya kuzuiwa kumuoa mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 22.

Familia ya marehemu Lucy Boke imedai kuwa mshukiwa alikasirika kwa kuwa hangeweza kumuoa mwanadada huyo kwa vile walikuwa na uhusiano wa kinasaba.

Familia zote mbili, ya Boke na ya Orengo, zilikutana na kukubaliana kwamba wawili hao hawataoana licha ya kuwa walikuwa na mtoto pamoja, jambo ambalo lilimkasirisha mshukiwa anayeripotiwa kumfuata mzazi huyo mwenzak hadi Jogoo Estate, mjini Kisii alikokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kisii National Polytechnic na kudaiwa kumuua.

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 22 alitoka katika kijiji cha Masaba, Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori, sawa na mshukiwa.

Mama wa marehemu Lucy Boke, Bi Amina Nyihembe aliviambia vyombo vya habari kuwa bintiye alikataa ombi la mzazi huyo mwenzake la kutaka kuolewa naye.

"Lucy alikuwa amejitahidi kusoma na sasa amekufa kwa sababu ya mapenzi. Hatuwezi kuamini hili,” Bi Nyihembe alisema.

Mjombake marehemu, Bw Ngen Matatiro alisema familia zilikutana na kukubaliana kwamba wawili hao hawangeoana kwani kuoa mwanafamilia katika jamii yao ni chukizo.

Aidha, inaarifiwa kuwa mzozo mpya pia umeibuka kuhusu mahali ambapo marehemu Lucy Boke atazikwa. Familia ya mshukiwa inadai mwili huo huku familia ile ya Boke ikisema wawili hao hawakuwa wameoana ili kuidhinisha hilo.

Familia ya Boke imekataa madai hayo.

Stephen Orengo alinusurika kifo Alhamisi jioni wakati polisi walipomuokoa kutoka kwa umati wenye hasira wa wanafunzi waliokuwa wakitaka kumuangamiza kwa madai ya kumuua Lucy Boke ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Mshukiwa huyo alisemekana kumfuata msichana huyo hadi nyumbani kwake katika mtaa wa  Jogoo Estate, mjini na kumuua ndani ya nyumba yake. Inasemekana alisafiri umbali mrefu kutoka nyumbani kwao Kaunti ya Migori hadi Kisii kutekeleza uhalifu huo kufuatia mzozo wa kimapenzi baina yao.

Majirani waliosikia kilio cha marehemu hawakuweza kuokoa maisha yake wakati wa tukio hilo la kuhuzunisha na mwili wake uliokuwa umejeruhiwa vibaya ulipatikana ndani ya chumba chake. Kulikuwa na dalili za mapambano na madoa ya damu ndani ya nyumba, ishara kuwa marehemu alijaribu kupigania maisha yake kabla ya Orengo kufanikiwa kumdunga kisu mara kadhaa na kusababisha kifo chake cha uchungu