Tunakuonea 18, hakuna Handshake! DP Gachagua amfokea Raila Odinga

Wewe aufanye kazi yako ya upinzani, uende uulize maswali, upige kelele, ukae huko utukosoe ukiwa uko mbali - Gachagua alisema.

Muhtasari

• Gachagua alisema Odinga alitumia woga kama huo kwa rais mstaafu Kenyatta mpaka akafaidi kwa Handshake.

• Haya yanajiri huku Odinga na kambi yake wakiandaa maandamano Jumatano wiki hii kupinga kufukuzwa kazi kwa makamishna 4 wa IEBC.

DP azidi kumshambulia Odinga vikali
DP azidi kumshambulia Odinga vikali
Image: Facebook

Naibu wa rais Rigathi Gachagua ameendeleza mashambulizi yake vikali dhidi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kufuatia mpango wake wa kuandaa maandamano kuanzia Jumatano wiki hii kupinga kutimuliwa kazi kwa makamishna wane wa tume ya IEBC.

Gachagua alikuwa anazungumza Jumapili katika ibada ya kanisa ambapo alisema kuwa walikuwa wanajua Odinga hajabadilika hata baada ya kubembelezwa kukubali hivyo na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Sisi tulikuwa tunasukumiwa yule mzee, lakini sisi tulimuelewa na tukasema bado hajabadilika. Rais wa zamani akasema amebadilika tukakataa kabisa. Sasa amerudi kwa yale maneno yake, ati aliibiwa kura,” Gachagua alisema.

DP alisema kuwa bado wanamjua Odinga na njama zake zote na kumuomba rais Ruto kuwa katu hawataki awaletee handshake nyingine naye, huku akisema kuwa wanamtazama kwa mbali.

“Mtukufu rais, huyu mzee sisi tunamjua, sisi tunamuonea inaitwa 18. Na sisi ni marafiki wako rais na unajua. Tutakuambia ukweli kila siku kuwa huyu mzee hatumtaki, ameanza lugha ya maandamano eti auzie rais wetu woga ili aitwe kwa handshake. Rais tunakuomba, sisi tumechangia pakubwa kwa hii serikali, sisi hatumtaki kwa serikali yetu,” Gachagua alisema.

Naibu rais alisema kuwa hawapingi Odinga kuendesha shughuli zake za upinzani bali kile hawataki kabisa ni kuanzisha maandamano ili kumrubuni rais Ruto kumuita kwa ajili ya maridhiano kama ambavyo alimfanyia rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Yeye afanye kazi yake ya upinzani, aende aulize maswali, apige kelele, akae huko atukosoe akiwa uko mbali,” Gachagua alisema.