Daktari akamatwa kwa kumsaidia msichana kuavya - Ngara

Muhtasari

• Vifaa na vijusi kadhaa vilipatikana katika kliniki

• Polisi walidokezewa na wananchi kuhusu kilichokuwa kinafanyika 

• Wasichana wengine 2 walikiri kulipa shilingi 12,000 na 10,000 kutoa mimba 

Jonah Kipsiror Morori akiwa ameshika chombo kilichobeba vijusi alipokamatwa katika Prestige Health Points Medical Centre mjini Nairobi Oktoba 15, 2020. picha: GEORGE OWITI
Jonah Kipsiror Morori akiwa ameshika chombo kilichobeba vijusi alipokamatwa katika Prestige Health Points Medical Centre mjini Nairobi Oktoba 15, 2020. picha: GEORGE OWITI

Taarifa ya George Owiti 

Daktari anayedaiwa kufumaniwa akisaidia msichana kuavya mimba  mjini Nairobi amekamatwa. 

Jonah Morori wa kituo cha matibabu cha Prestige Health Points Medical Centre alikamatwa pamoja na mwenzake, wauguzi watatu na msichana anayedaiwa kuavya mimba mtaani Ngara mjini Nairobi siku ya Alhamisi. 

Maafisa wa polisi kutoka Pangani waliwatia mbaroni washukiwa baada ya kudokezewa na wananchi kuhusu kilichokuwa kikiendelea.   

Maafisa hao walinasa vifaa vilivyotumiwa kutekeleza uavyaji mimba na vijusi kadhaa.

Wasichana wawili waliopatikana katika kliniki hiyo walisema kwamba walikuwa wameavya mimba. Mmoja alidai kulipa shilingi elfu 12 na mwingine shilingi elfu 10. 

Baada ya kuhojiwa, Morori alisema kwamba hospitali hiyo inamilikiwa na mwanamke mmoja na huendeshwa na madaktari watatu akiwa mmoja wao.

Naibu afisa mkuu wa polisi William Sirengo alisema kwamba sita hao wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha pangani.

“Wanaume hao hawajaonyesha stakabadhi zozote kuonyesha wao ni madaktari. Hawana nambari za usajili,” alisema.

msichana aliyekamatwa atapelekwa kufanyiwa uchunguzi wa matibabu kabla ya washukiwa kufikishwa mahakamani. 

Duru ziliarifu The Star kwamba kliniki hiyo imekuwa ikihudumu kwa miaka saba sasa.