Makaribisho ya Uhuru kwa mkutano wa mawaziri Manyani yaibua hisia

Muhtasari

• Ruto asalia kuwa mtazamaji huku Matiang'i akimlaki rais Kenyatta

• Kulingana na itifaki naibu rais William Ruto ndiye anayefaa kumlaki rais

• Mkutano unafanyika katika chuo cha KWS Manyani 

Rais Uhuru Kenyatta akiwasili chuo cha Manyani na kulakiwa na waziri Fred Matiang'i huku naibu rais William Ruto akitazama. PICHA/PSCU
Rais Uhuru Kenyatta akiwasili chuo cha Manyani na kulakiwa na waziri Fred Matiang'i huku naibu rais William Ruto akitazama. PICHA/PSCU

Makaribisho ya rais Uhuru Kenyatta alipowasili katika chuo cha mafunzo ya maafisa wa huduma kwa wanyama pori eneo la Manyani yameibua mjadala mkali nchini.

Kulingana na picha za kitengo cha habari cha rais PSCU rais Kenyatta alipowasili alilakiwa na waziri wa masuala ya ndani Fred Matiang'i huku naibu rais William Ruto akitazana na kusubiri zamu yake kumsalimu rais.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alikuwa wa kwanza kuweka picha ya rais Kenyatta akiwasili na kulakiwa na Matiang'i huku Ruto akitazama na kumkejeli Matiang'i  kwamba;

"The Deputy President Fred Matiangi receiving the President thereafter introduce other Cabinet members. Those of us who didn’t witness the last days of Mzee Jomo Kenyatta ‘will see things’ in the next 22 months" (Naibu rais Fred Matiang'i akimlaki rais kisha baadaye awatambulishe mawaziri. Sisi ambao hatukuwepo siku za mwisho za mzee Jomo Kenyatta tutaona mambo kwa kipindi cha miezi 22 ijayo).

Kulingana na itifaki naibu rais William Ruto ndiye anayefaa kumlaki rais.

Rais Kenyatta anaongoza mkutano wa mawaziri katika chuo cha Manyani kujadili masuala mbali mbali katika serikali. 

Mkutano huo pia unatarajiwa kuzamia ripoti ya BBI  ambayo inatarajiwa kutolewa na rais wakati wowote.

Naibu rais William Ruto amekuwa katika mstari wa mbele akisema kwamba hataunga mkono mchakato wa BBI ambao lengo lake kuu ni kutafutia wanasiasa nyadhifa za uongozi na ilhali wakenya wengi hawana ajira.

Mawaziri wote walisafirishwa katika eneo la Manyani kwa ndege kutoka uwanja wa ndege wa Wilson kwa ndege za kijeshi kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huOu pia unalenga kuleta pamoja baraza la mawaziri ili mawaziri wote wazungumze kwa kauli moja na kudumisha mshikamano serikalini.