Wakenya wahimizwa kupimwa mapema saratani na kutibiwa

Muhtasari

•  Bi Kenyatta amewahimiza Wakenya kupimwa mapema na kupata matibabu.

• Mama wa Taifa aliwatambua waathiriwa wa saratani na kuwapa moyo wale wanaougua maradhi hayo.

• Hafla ya kuadhimisha mwezi wa ufahamu kuhusu saratani ya matiti ilifanyika katika kaunti ya Makueni

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta
Mama wa Taifa Margaret Kenyatta

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta amewahimiza Wakenya kupimwa mapema na kupata matibabu kama hatua ya kushinda vita dhidi ya saratani.

Bi Kenyatta siku ya Alhamisi alitilia mkazo usaidizi wake kwenye juhudi zinazoendelea kueneza habari kuhusu saratani ya matiti ili kuokoa maisha ya wanawake kupitia mpango wa shirika lake la Beyond Zero.

“Tunafahamu umuhimu wa kupimwa mapema, manufaa ya kutambua maradhi hayo kwa wakati na matibabu, na vile haya yanaimairisha kiwango cha kunusurika na kuendeleza juhudi zetu za pamoja katika kukabiliana na ongezeko la visa vya saratani miongoni mwa jamii zetu,” kasema Mama wa Taifa.

 

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha mwezi wa Oktoba wa kueneza ufahamu kuhusu saratani, Mama wa Taifa aliwatambua waathiriwa wa saratani na kuwapa moyo wale wanaougua maradhi hayo huku akipongeza familia zao kwa kusimama kidete nao.

"Aidha ni mwezi ambapo tunatilia mkazo usaidizi na kuungana na wanawake jasiri, ambao wamejitokeza kujitambulisha na kutoa ufahamu kuhusu safari zao za kipekee. Tunawapongeza kwa sababu kupitia sauti zenu, tumesikia hadithi zenu za kunusurika,” kasema Mama wa Taifa.

Mama wa Taifa alisisitiza kwamba ufahamu pamoja na kuenezwa kwa habari hizi na maamuzi ya afya kwa wakati husaidia kupunguza maumivu na mzigo wa saratani na maradhi mengine kwa ujumla.

Wakati huo huo, hafla ya kuadhimisha mwezi wa ufahamu kuhusu saratani ya matiti ilifanyika siku ya Alhamisi katika kaunti ya Makueni kwa kuzinduliwa kliniki ya saratani katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Makueni iliyojengwa kupitia mradi wa chama cha Wake wa Magavana wa kaunti.

Kliniki hiyo ya saratani kwa jina “Chumba cha Zambarau” inapeleka karibu huduma za upimaji, kutambua na kutibu ugonjwa huu karibu na wananchi wa Makueni.