Uhuru amwomboleza aliyekuwa Kamishna wa Polisi Duncan Wachira

Muhtasari

• Wachira alifariki akiwa nyumbani kwake mapema siku ya Jumatano

• Alihudumu kama kamishna wa polisi katika ya mwaka 1996 na 1998

• Uhuru alimkumbuka Wachira kuwa mtumishi na mzalendo halisi wa taifa la Kenya 

Aliyekuwa kamishna wa polisi Duncan Wachira. picha: HISANI
Aliyekuwa kamishna wa polisi Duncan Wachira. picha: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambi rambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa  aliyekuwa Kamishna wa Polisi Duncan Wachira ambaye alifariki mapema siku ya Jumatano nyumbani mwake Jijini Nairobi.

Katika risala yake, Kenyatta  alimkumbuka mkuu huyo wa zamani wa polisi kuwa mtumishi na mzalendo halisi wa taifa la Kenya aliyejitolea kwa maslahi ya nchi.

“Nimemjua Duncan Wachira kuwa mtu mwenye hekima kubwa na sifa ya kipekee. Nyakati zake kama mkuu wa huduma ya polisi, Wachira alianzisha mabadiliko ambayo yaliboresha  maslahi ya maafisa wa polisi.

"Bw. Wachira pia anakumbukwa kwa msimamo wake mkali katika vita  dhidi ya uhalifu Jijini Nairobi. Nyakati zake akiwa mkuu wa polisi, nakumbuka kwamba makundi mengi ya uhalifu yalikomeshwa," Rais aliomboleza.

Kiongozi wa Taifa alisema maadili ya marehemu Wachira ya bidii na kujitolea kazini yatadumu kuwahimiza  Wakenya wengi vijana hasa wale wanaohudumu katika vikosi vya usalama nchini.

Rais alimuomba Mwenyezi Mungu kuipa familia ya Bw. Wachira nguvu na faraja za kuhimili msiba huo.

Wachira alifariki akiwa nyumbani kwake mjini Nairobi baada ya kuugua. Alihudumu kama kamishna wa polisi kati ya mwaka 1996 na 1998 chini ya utawala wa rais mustaafu hayati Daniel Moi.