Uhuru awajibu wanaopinga BBI

Muhtasari

• Rais aeleza umuhimu wa BBI 

• Swali hili la“ Sisi dhidi ya wao” sharti likomeshwe

• Aonya dhidi ya kampeini za mapema 

Rais Uhuru Kenyatta asalimia wananchi mjini Kisii siku ya Mashujaa. Picha:PSCU
Rais Uhuru Kenyatta asalimia wananchi mjini Kisii siku ya Mashujaa. Picha:PSCU

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumanne alitoa wito wa maafikiano ya kikatiba ambayo yatajumuisha jamii za makabila yote na kuthibiti usawa na umoja wa kitaifa.

Akisema kwamba taifa hili limefikia wakati wa kufanya mabadiliko ya kikatiba, Rais Kenyatta alikariri tahadhari dhidi ya hali ya kutopindika ambayo inazua siasa mbaya na za migawanyiko.

“Waanzilishi wetu wa Taifa na Mashujaa wa Kikatiba hawakunuia kwamba utaratibu wa kikatiba utufanye kuwa watumwa. Waliutengeneza ili kututumikia. Na ulipofika mwisho wa kututumikia, tulistahili kuiga mfano wa Waanzilishi wa Taifa na kuufikiria upya,” kasema Rais Kenyatta.

 

Kiongozi wa Taifa alisema haya katika uwanja wa michezo wa Gusii katika kaunti ya Kisii alipoongoza taifa katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku kuu ya Mashujaa.

Rais alisema anatetea maafikiano ya kikatiba ambayo yatathibiti kanuni za kidemokrasia nchini bila ya kuleta mgawanyiko wa uanuwai wa taifa la Kenya.

“Swali hili la“ Sisi dhidi ya wao” sharti likomeshwe. Na tunapotimiza haki zetu za kidemokrasia, kamwe hazipaswi kuvuruga uanuwai wetu. Sharti kanuni muhimu kuwa umoja katika uanuwai wetu,” kasema Rais Kenyatta.

Rais aliwahimiza Wakenya waafikiane kikatiba kwa kuzingatia masuali matatu ya kitaifa ambayo yatashughulikia ujumuishaji wa kisiasa, usawa katika utoaji nafasi na raslimali, mbali na kushughulikia mabishano na ghasia ambazo hutokea kila baada ya msimu wa uchaguzi.

“Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, uchumi hudidimia kwani inatarajiwa kutakuwa na mabishano na vurugu za uchaguzi. Na mwaka mmoja baada ya uchaguzi, shughuli za uchumi bado hazijashika kasi kwani masoko yanaendelea kushughulika na makundi mbali mbali ya kisiasa yanayochipuka.

“Hii inamaanisha kwamba katika kila msimu wa uchaguzi wa miaka mitano, miaka miwili hupotea kwa kushughulikia tu masuala ya uchaguzi,” kasema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alionya kwamba kampeini za mapema na hali ya uchaguzi wa kila mara inazua wasiwasi na kuinyima nchi hii mazingira ambako biashara zinaweza kuimarika kwa kuvutia mtaji wa kila wakati.

 

“Kusema kweli, haya siyo yale wanaharakati wa katiba wakati wa uhuru walitutakia. Na tusipobadilika wakati huu, tukiwa na muda wa maafikiano ya kikatiba, tatizo hili litaendelea kuvuruga nchi yetu kwa miaka mingi. 

“Hivyo basi, mwaliko wangu kwa Taifa ni kuwa na mazungumzo wazi na ya kweli kuhusu suala hili. Na hatupaswi kuogopa kufanya maamuzi ya kijasiri kama walivyofanya Waanzilishi wa Taifa hili,” kasema Rais.