Uhuru na Raila wapokea ripoti ya BBI

Muhtasari

• Uhuru alisema ripoti hiyo inagusia maswala mbali mbali muhimu yanayoathiri taifa la Kenya.

•Rais alisema huu si wakati wa kuleta migawanyiko bali  ni wakati wa kuonyesha uongoz.

• Raila alisema ripoti hiyo ndio njia mwafaka ya kukomboa Kenya na kuondoa ukabila.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakipokea ripoti ya BBI. Picha: ANGWENYI GICHANA
Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakipokea ripoti ya BBI. Picha: ANGWENYI GICHANA

Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga wamepokea ripoti ya BBI katika hafla iliyofanyika katika ikulu ndogo ya Kisii. 

Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba ripoti hiyo inagusia maswala mbali mbali muhimu yanayoathiri taifa la Kenya.

Rais alisema wakenya hawafai kupoteza fursa hii ambapo kuna mazingira bora ya kufanyia mabadiliko katiba kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

 

Alitoa wito wa maafikiano ya kikatiba ambayo yatajumuisha jamii na makabila yote na kuthibiti usawa na umoja wa kitaifa.

"Huu si wakati wa kuleta migawanyiko, huu ni wakati wa kuonyesha uongozi, ni wakati wa kuleta nchi pamoja'" Rais Kenyatta alisema.

Rais aliongeza kuwa..."Mimi na ndungu yangu hii ndio mara ya kwanza pia sisi tunaipokea ripoti hii na ndio maana sijakuwa nikiongea kuihusu nilitaka niisome kwanza".

Uhuru aliagiza kamati iliyoongoza mchakato wa BBI kuhakikisha kwamba ripioti hiyo imesambazwa kwa wakenya wengi kabla ya siku ya Jumatatu watakapoichambua katika ukumbi wa Bomas of Kenya. 

"Kile tunatafuta ni stakabadhi ya vizazi vijavyo, mimi sio rais wa mwisho wa Kenya watakuja marais wengi lakini Kenya itasalia ile ile," rais Kenyatta alisema.

Akihutubia hafla hiyo kinara wa upinzani Raila Odinga alimepuuzilia mbali wale waliokuwa wakipinga mchakato wa BBI akisema kwamba ripoti hiyo imezingatia maoni ya wakenya kutoka pembe zote za nchi.

Raila alisema ripoti hiyo ndio njia mwafaka ya kukomboa Kenya na kuondoa ukabila na kutengwa kwa baadhi ya maeneo.

 

Alisema kwamba Kenya mpya lazima izaliwe kikatiba. Alipinga vikali madai kwamba ripiti hiyo inalenga kumfanya rais Uhuru kuwa waziri mkuu na yeye kuwa rais.

Alisema katiba ya Kenya kama tu zingine inafaa kufanyiwa marekebisho ili kuiana na matakwa ya wakenya.

"Wewe sema yako na sisi tuseme yetu, wakenya wataamua na tutafuata uamuzi wao," Raila alisema.

Raila alikashifu viongozi wanaoligawanya taifa kwa misingi ya matajiri na maskini akisema kwamba baadhi ya watu wanaoongoza mjadala huu wamekuwepo katika serikali na wangeweka mikakati ya kuboresha maisha ya wakenya

"...eti saa hii ndio wamejua kwamba kuna watu wanaohitaji mikokoteni".