Aisha Jumwa afikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji

Muhtasari

• Wanadaiwa kuvamia mkutano wa kisiasa eneo la Ganda na kupelekea kupigwa risasi na kuuawa kwa Gumbao Jola aliyekuwa na umri wa miaka 48.

• Wamekuwa wakizuiliwa tangu siku ya Jumatatu 

•Wawili hao wanatarajiwa kuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Washukiwa Geoffrey Otieno na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wakiwa kizimbani.Picha: Maktaba
Washukiwa Geoffrey Otieno na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wakiwa kizimbani.Picha: Maktaba

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa  na mshukiwa mwenza Geoffrey Otieno wanatarajiwa kukubali au kukataa mashtaka ya mauaji dhidi yao hivi leo.

Ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashataka ya umma iliidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya Jumwa na Otieno baada ya kukubaliana na ushahidi uliowasilishwa na maafisa wa upelelezi. Wanakabiliwa na shtaka la kumuua mwanamume mmoja katika kaunti ya Kilifi Oktoba mwaka jana.

Wawili hao wanatarajiwa kuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Jaji wa mahakama kuu mjini Mombasa Njoki Mwangi aliamuru wawili hao kuzuiliwa na polisi katika kituo cha polisi cha Port mjini Mombasa kwa siku tatu ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kurejeshwa mahakamani siku ya Alhamisi.

Wanadaiwa kwamba Oktoba tarehe 29 katika ghasia zilizozuka eneo la Ganda walivamia mkutano wa kisiasa eneo la Ganda na kupelekea kupigwa risasi na kuauwa kwa Gumbao Jola aliyekuwa na umri wa miaka 48.

Kwingineko,

Washukiwa watatu wa ujambazi raia wa kigeni wanafikishwa mahakamani leo (Alhamisi).

Washukiwa walitiwa mbaroni siku ya Jumatatu na bunduki aina ya AK47 kupatikana.

Walikamatwa baada ya lori kushambuliwa kwa risasi na kulazimika kusimama lilipokuwa likielekea eneo la Shompole.

Kisha waliwaibia watu saba waliokuwa ndani ya lori hilo na kujaribu kutorokea katika gari ndogo gari. Gari walimokuwa wakijaibu kutorokea pia lilinaswa na polisi.