Hukumu ya washukiwa wa shambulizi la Westgate yaahirishwa

Washukiwa wa shambulizi la Westgate
Washukiwa wa shambulizi la Westgate

Kutolewa kwa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa shambulizi la kigaidi la Westagte imeahirishwa hadi Ijumaa wiki ijayo. 

Hii ni baada ya afisa wa kutathmini tabia za washukiwa kuambia mahakama siku ya Alhamisi kuwa ripoti yake ilikuwa haijakamilika kwa sababu bado hajawahoji baadhi ya wahasiriwa. 

Afisa huyo Peter Macharia alisema kwamba tayari wameawahoji washukiwa hao wawili Mohammed Ahmed na Hussein Hassan Mustafa.  

Pia alisema kwamba tarayi alikuwa amezungumza na jamaa za washukiwa na mhasiriwa mmoja wa Westgate. 

Macharia alisema ripoti yake itakuwa tayari ifikiapo wiki ijayo ili kumwezesha hakimu kutoa hukumu yake dhidi ya washukiwa hao wawili. 

Mahakama hata hivyo, iliagiza vyombo vya habari kutochapisha au kupeperusha taarifa zozote za wahasiriwa zilizowasilishwa mahakamani. 

Hakimu mkuu Francis Andayi alionya wanahabari kutochapisha taarifa hizo. 

Taarifa hizo zitasaidia kuafikia uamuzi kuhusu hukumu ya watuhumiwa. 

Wawili hao mapema mwezi huu walipatikana na hatia ya kushirikiana kutekeleza shughuli za kigaidi. 

Mmoja wa washukiwa Liban Abdullahi Omar aliondolewa mashtaka dhidi yake kwa kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha lakini baadaye akatekwa nyara punde tu alipoachiliwa huru.