Ruto si maskini Joho awambia wafuasi wa naibu rais

Muhtasari

•Joho alidai kwamba Ruto anachochea uhasama miongoni mwa wakenya 

•Naibu rais analenga kusambaratisha mchakato wa BBI 

•Ruto amekuwa akizunguka na mahelikopta 

Gavana wa Mombasa Hassan Joho na naibu rais William Ruto. Picha /MAKTABA
Gavana wa Mombasa Hassan Joho na naibu rais William Ruto. Picha /MAKTABA

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amekosoa vuguvugu la 'hustler' lake naibu rais William Ruto akisema kwamba litagawanya wakenya.

Joho alisema kwamba vuguvugu hilo linalenga kuibua uhasama baina ya maskini na matajiri, mgawanyiko ambao rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga wanajaribu kuondoa kupitia mchakato wa BBI.

“Ni makosa kwa viongozi kucheza na hisia za watu kwa sababu wanataka kuchaguliwa. Najihusisha na BBI kwa sababu nataka Kenya yenye umoja,” Joho alisema.

Joho alisema kwamba Ruto alikuwa akicheza na hisia za watu maskini, akiongeza kuwa naibu rais alikuwa anachochea hisia za watu ili aligawanye taifa na hatimaye kusambaratisha mchakato wa BBI.

Alisema umaskini sio kitu cha kujivunia na watu hawafai kuutukuza au kuutumia kupata mamlaka. Alisema Ruto alikuwa anawaziba macho wakenya.

“Huwezi niambia, kwa tafsiri zote, kuwa naibu rais wa Jamhuri ya Kenya ni maskini,” Joho alisema. 

“Unasemaje wewe ni maskini na ilhali unapaa kila mahali na helikopta tano?”

Katika hotuba yake siku ya mashujaa mjini Kisii, Ruto alisema kwamba kuna umuhimu wa kuleta pamoja kila mtu ili kufanikisha azimio la umoja wa kitaifa.

Ruto alitoa wito pawepo mjadala ili kujumuisha maoni ya kila mkenya katika mchakato wa BBI.

Joho alisema kwamba lengo la BBI ni kuboresha maisha ya usoni ya wakenya.

Alisema Ruto amekuwa akieneza uongo kuwa BBI inalenga kunufaisha wachache, madai aliosema ni ya uongo.

Alisema BBI inalenga kuongeza mgao wa serikali za kaunti hadi asilimia 35 kutoka asilimia 15 “…halafu mtu anakuambia ukatae pendekezo hili?”

Kulingana na Joho mapendekezo ya BBI yatawapa wakenya nafasi nyingi za kujiendeleza kuliko mikokoteni alikuwa akipeana naibu rais.