Janga la Covid: Wagonjwa kulazwa kwenye hoteli Kenya

Muhtasari

•Alhamisi visa 1,068 viliripotiwa kutoka kwa sampuni 7,556 ambacho ni kiwango cha maambukizi cha asilimia 14.13.

• Jumla ya vitanda 200,000 vilivyokuwa vikitumika kuwatenga wagonjwa havipo baada ya kufunguliwa kwa shule.

•Hoteli 40 zilizokuwa zikitumika kama maeneo ya kutengwa kwa wagonjwa zimerejelea shughuli zao za kawaida.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe
Waziri wa afya Mutahi Kagwe

Taarifa ya John Muchangi 

Kuna hofu kwamba Kenya inaelekea katika awamu ya pili ya janga la Covid-19 huku idadi ya maambukizi inayotangazwa na wizara ya afya ikiwa ya kutamausha. 

Siku ya Alhamisi visa 1,068 viliripotiwa kutoka kwa sampuni 7,556 ambacho ni kiwango cha maambukizi cha asilimia 14.13.

 

Kenya pia imesajili idadi ya juu zaidi ya vifo kwa wiki moja huku jumla ya watu 65 wakifariki kutokana na Covid-19 na kufikisha jumla ya watu 870 waliofariki kutokana na virusi hivi. 

Leo ni wiki ya 33 tangu kisa cha kwanza  cha Covid-19 kuripotiwa nchini, Machi 13 mwaka huu.

Kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi wizara ya afya sasa imeanza kufanya mazungumzo na zaidi ya hoteli 20 kutumika kulaza wagonjwa wa covid-19 na pia kutumika kama maeneo ya kutenga wagonjwa ili kuondolea hospitali shinikizo kutokana na idadi kubwa ya maambukizi kwa sasa. 

Huku kukiwepo hofu kuwa huenda nchi inaelekea kwa awamu ya pili ya janga la Covid-19,  serikali inatafuta kujiandaa kwa chochote huku baadhi ya taasisi za kibinafsi zikiwa tayari zimejaa.

Baraza la maafisa wa matibabu, wanafamasia na madaktari wa meno lilisema kwamba taifa sasa lina jumla ya vitanda maalum vya wagonjwa wa covid 18,443. Afisa mkuu mtendaji Daniel Yumbya alisema vitanda hivyo vinatosha kwa sasa lakini huenda vitanda zaidi vikahitajika ikiwa maambukizi yataendelea kupanda kwa kiwango cha sasa. 

Kulingana na baraza hilo jumla ya vitanda laki mbili vilivyokuwa vikitumika kuwatenga wagonjwa wa covid-19 sasa havipo kutokana na  hatua ya kufunguliwa kwa shule kwa awamu.

Takriban hoteli 40 zilizokuwa zikitumika kama maeneo ya kutengwa kwa wagonjwa wa covid pia tayari zimesitisha shughuli hiyo na kuanza shughuli zao za kawaida.  

 

"Tumerejelea mazungumzo yetu na hoteli za kibinafsi kuwatoza bei nafuu wagonjwa waliotengwa. Hatutaki hospitali zishindwe kuhimili idadi kubwa ya wagonjwa  ," Yumbya alisema.  

Hata hivyo alisema wale wagonjwa ambayo watawekwa  katika hoteli ni wale ambao hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo, hawawezi kujitenga wakiwa nyumbani na pia wana uwezo kulipia gharama zilizopunguzwa za kukaa kwa hoteli.