Uhuru aidhinisha mswada wa kuteuliwa kwa makamishna wa IEBC

Muhtasari

•Mswada wa mageuzi nambari 3 wa mwaka wa 2019 wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC).

•Sheria hiyo mpya inatoa vigezo vya uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na inabainisha ujuzi 

 

Rais Kenyatta akitia saini mswada wa Tume ya IEBC na ule wa Matangazo ya Bidhaa na Huduma nyanjani katika Kaunti. Picha:PSCU.
Rais Kenyatta akitia saini mswada wa Tume ya IEBC na ule wa Matangazo ya Bidhaa na Huduma nyanjani katika Kaunti. Picha:PSCU.

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano alitia saini kuwa sheria mswada wa mageuzi nambari 3 wa mwaka wa 2019 wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC).

Rais pia allidhinisha mswada wa Kaunti wa uthibiti wa Matangazo ya Bidhaa na Huduma kupitia vibao vya nyanjani wa mwaka 2020.

Sheria hiyo ya mageuzi ya Tume ya IEBC inabuni kamati maalum ya kusimamia kujazwa kwa nafasi zinazoachwa wazi katika tume hiyo na pia uteuzi wa makamishna wa tume hiyo katika siku zijazo.

Sheria hiyo mpya inatoa vigezo vya uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na inabainisha ujuzi unaohitajika wa wanachama wa kamati hiyo ya kuwachagua.

Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi

Sheria ya kudhibiti Matangazo ya Nyajani katika Kaunti inanuia kurahisisha utangazaji wa bidhaa na huduma nyanjani katika kaunti kwa kuhakikisha usawa katika masuala ya kibiashara, kimazingira na usalama wa umma.

Sheria hiyo inatambua umuhimu unaoendelea kukua wa matangazo ya nyanjani kama njia moja ya kuziletea mapato serikali za kaunti na kuleta usawa katika utoaji wa leseni kote katika kaunti 47.

Miswada hiyo iliwasilishwa kwa Rais katika Ikulu ya Nairobi na Mwanasheria Mkuu wa serikali Ken Ogeto na kushuhudiwa na Spika wa Seneti Ken Lusaka na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.