Sayansi na utafiti

Sayansi na utafiti ni muhimu katika kuimarisha uwezo kamili wa maendeleo nchini-Rais Uhuru

Rais alisema serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za utafiti

Muhtasari

 

  • Rais Kenyatta alisema hayo leo wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya kituo cha kimataifa cha utafiti kuhusu wadudu (ICIPE) Jijini Nairobi
  • Alisema sharti Afrika iendelee kupanua uekezaji wake katika sayansi na utafiti ili kuiwezesha kuafikia matarajio ya kuwa bara lenye ustawi na amani.

 

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

  Na  PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema kwamba sayansi na utafiti ni nguzo muhimu katika kuimarisha uwezo kamili wa maendeleo nchini hasa katika kutafuta suluhisho za changamoto zinazokabili ustawi wa Kenya.

Hivyo basi, Rais alisema Serikali itaendelea kutekeleza mipango inayonuiwa kuimarisha talanta zinazochipuka ili kuwawezesha wananchi kuchuma mali na kupanua nafasi za ajira kwa Wakenya.

Rais Kenyatta alisema hayo leo wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya kituo cha kimataifa cha utafiti kuhusu wadudu (ICIPE) Jijini Nairobi

Katika hotuba yake iliyorekodiwa kwa video, Kiongozi wa Taifa alipongeza ICIPE kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sayansi na utafiti barani Afrika katika miaka hamsini iliyopita.

“Huku taasisi hii inaposherehekea miaka 50 ya huduma, kwa kushirikiana na serikali kote barani, tunatambua jukumu kuu mliotekeleza na mnaloendelea kutekeleza, katika utafiti wa wadudu, afya ya mimea, afya ya wanyama, afya ya mazingira, kwa nia ya kuboresha afya na maslahi ya wanadamu,” kasema Rais.

Alisema sharti Afrika iendelee kupanua uekezaji wake katika sayansi na utafiti ili kuiwezesha kuafikia matarajio ya kuwa bara lenye ustawi na amani.

“Hakika, Afrika itaendelea kutegemea mashirika ya kisayansi sio tu kushughulikia changamoto za maendeleo za sasa na siku zijazo lakini pia ili kuwa jukwaa la kutuwezesha kutumia fursa zinazojitokeza katika sekta za kidijitali na kibayolojia,” kasema Rais.

Rais alisifu mipango ya mafunzo ya ICIPE inayotolewa kupitia Mpango wa Kanda wa Masomo ya Uzamili katika Sayansi ya Wadudu na vile vile Mpango wa Utafiti wa Wanafunzi, akisema juhudi hizi zimesaidia kungoeza mno idadi ya wanasayansi na watafiti katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 “Vivyo hivyo, natambua kwamba mnamo mwaka wa 2008, ICIPE ilichaguliwa na mataifa ya Afrika kusimamia Hazina ya Kanda ya Masomo na Ubunifu kupitia Ushirikiano katika Ujuzi wa Sayansi Tekelezi, Uhandisi na Teknolojia. Nia kuu ya hazina hiyo ni kutoa mafunzo kwa hadi wanasayansi 1000 katika kiwango cha masomo ya uzamifu kila mwaka kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika nyanja kadha muhimu za kisayansi,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema Ruwaza ya Maendeleo ya Kenya kufikia Mwaka 2030 pamoja na Ajenda ya Muungano wa Afrika ya Mwaka 2063 zote zinatambua wajibu muhimu unaotekelezwa na sayansi na taasisi za kisayansi kama vile ICIPE katika kuafikia malengo ya maendeleo.

Kutokana na elimu hii, Rais alisema serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za utafiti kama washirika muhimu wa maendeleo huku akiongeza kwamba serikali ya Kenya imechangia zaidi ya shilingi milioni 200 kwa Hazina ya Kanda ya Ufadhili wa Masomo na Ubunifu wa Ushirikiano wa Maarifa katika Sayansi tekelezi, Uhandisi na Teknolojia ambako yeye ndiye mwenyekiti wa sasa.

“Mchango wetu kwa misingi hii unawiana na Ruwaza ya Maendeleo kufikia mwaka 2030, Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Kudumu pamoja na Ajenda ya Muungano wa Afrika ya mwaka 2063,” kasisitiza Rais.

Kiongozi wa Taifa alitoa hakikisho kwamba serikali itaendelea kutekeleza sera za maendeleo ili kuendeleza sayansi na ubunifu sio tu kama chombo cha ukuaji wa kiuchumi bali pia njia ya kushughulikia ukosefu wa usawa wa kijamii.

“Tumetoa ahadi kuekeza hadi asilimia 2 ya bajeti yetu ya kila mwaka katika utafiti na ubunifu hatua ambayo inawiana na mipango yetu ya kitaifa ya maendeleo,” kasema Rais.

Rais alisema kwamba taasisi za sayansi na utafiti kama vile ICIPE ni washirika muhimu katika kutimiza matarajio ya Kenya ya maendeleo  yanavyofafanuliwa katika Ruwaza ya Maendeleo kufikia mwaka 2030 pamoja na mpango wa Nguzo Nne Kuu za Ajenda ya Maendeleo ambayo alisema inaenda sambamba na malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Kudumu.

“Hakika, ICIPE pamoja na taasisi nyingine za aina hiyo hapa nchini zimechangia maarifa muhimu ya kiufundi na elimu ya kisayansi ambayo yamedhihirisha kuwa muhimu kwa maendeleo yetu ya kitaifa.

“Mchango huu umesaidia kubuni nafasi bora za kazi, hususan kwa vijana waliohitimu, kuongeza fedha za kigeni kwa taifa hili na kuimarisha ushirikiano wetu, hasa katika nyanja ya elimu na utafiti ulimwenguni kote,” kasema Rais.

Kama sehemu ya sherehe hizo, Rais alizindua Ruwaza na Mkakati wa ICIPE kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, ambayo aliitaja kuwa bora na bayana huku akisema itaiweka taasisi hiyo katika nafasi nzuri ya uvumbuzi na kutoa suluhisho.

Mawaziri Raychelle Omamo wa Mashauri ya Nchi za Kigeni na Peter Munya wa Kilimo walipongeza taasisi ya ICIPE kutokana na kazi yake ya sayansi na utafiti ambayo walisema imekuwa muhimu katika kuyabadilisha maisha ya waafrika wengi.

Waziri Munya alisema taasisi ya ICIPE imetambulika ulimwenguni kutokana na kazi zake za utafiti ambazo zimesaidia wakulima kwa kiwango kikubwa kuimarisha faida za shughili zao.

“Kazi hii imefanya ICIPE kuwa maarufu barani Afrika kwa kuchangia juhudi za kutoa suluhisho kadha ambazo hazina maafa kwa wanyama, mimea na maisha ya binadamu,” kasema Waziri huyo wa Kilimo.

Wengine waliozungumza ni Mwenyekiti wa Baraza simamizi la ICIPE Prof Bill Hansson pamoja na Mkurugnezi Mkuu Dkt Segenet Kelemu.