Polisi aliyepigwa risasi na maharamia Meru, afariki

Muhtasari

Afisa huyo alifariki akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Nairobi.

Wenyeji wanafahamu waliotekeleza mashambulizi hayo.

Kaunti Kamishna wa Isiolo Herman Shambi (picha Gerald Mutethia)
Kaunti Kamishna wa Isiolo Herman Shambi (picha Gerald Mutethia)

Mmoja kati ya maafisa 11 wa polisi waliyopigwa risasi na maharamia wiki iliyopita amefariki kutokana na majeraha aliyokuwa amepata.

Kamishna wa kaunti ya Isiolo Herman Shambi alisema kwamba afisa huyo alifariki akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Nairobi. 

Shambi alitoa tahadhari kali dhidi ya majangili hao, akisema kwamba lazima wasalimishe bunduki zote haramu  wanazomiliki na  kila risasi iliyotumika kuwapiga risasi maafisa wa polisi ipatikane.

 

“Tunafikiri kuna nia mbaya katika uvamizi huo. Tumeanzisha msako na oparesheni ya kijasusi inaendelea kuwatafuta wahusika. Tuna baadhi ya majina. Inahuzunisha kuona maafisa wa kudumisha amani wasio na hatia wakivamiwa na mmoja wao kufariki. Lazima tuwatafute wahalifu wanakojificha,” alisema.

Shambi alisema kwamba maharamia hao hawafai kujificha au kuvuruga amani wakisingizia ukabila.  Alitoa wito kwa wenyeji kushirikiana nao ili kuhakikisha kwamba bunduki zote haramu zinasalimishwa. 

“KDF haihusiki katika oparesheni hii kama inavyodaiwa. Watu wanafaa kusalia watulivu na kuacha kupotoshwa na maharamia. Tunataka waliohusika, kwa sababu uvamizi huo ulidumu kwa zaidi ya saa mbili. 

Alisema wenyeji wanafahamu waliotekeleza shambulizi hilo.

Afisa mmoja amepoteza maisha, wenzake waliokuwa wamejeruhiwa tayari wameruhusiwa kuondoka hospitalini. 

Maafisa hao walishambuliwa walipokuwa wakishika doria katika eneo la Makinya, Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru. 

Walishambuliwa na zaidi ya maharamia 300.