Huduma namba kutumika kama kitambulisho - Matiang'i

Muhtasari

• Ifikiapo siku ya Jamhuri mwaka 2021 itakuwa lazima kwa kile mkenya kuwa na kadi ya Huduma.

• Serikali itachukuwa tahadhari itakapoanza zoezi la utoaji wa kadi za Huduma, kutokana na janga la Covid-19.

Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i, (Picha: Maktaba)
Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i, (Picha: Maktaba)

Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang’i amepigia debe Huduma Namba, akisema kwamba itaimarisha utoaji huduma za serikali.

"Watu wanahitaji serikali ili wapate huduma…Kwa muda nimekuwa serikalini uchungu watu hupitia kutafuta huduma huniuma sana…kuweka maelezo ya mtu kwa stakabadhi moja kulilenga kuondoa changamoto zilizoko," alisema.

"Naona, ikiwa bunge litaidhinisha, kadi ya Huduma ikitumika katika mchakato wa kukutambulisha wewe."

Matiang'i alisema haya katika mahojiano ya kipekee kwenye Citizen TV Jumatatu usiku.

Alisema serikali itachukuwa tahadhari itakapoanza zoezi la utoaji wa kadi za Huduma, kutokana na janga la Covid-19.

"Tutakuwa makini sana katika zoezi  la utoaji wa kadi za Huduma ili kuhakikisha kwamba tunazingatia masharti ya umbali wa mita moja …Kufikia siku kuu ya Jamhuri 2021, itakuwa lazima kwa maoni yangu, kuwa na kadi ya Huduma ili kupata huduma za serikali," Matiang'i alisema.

Kuhusu mchakato wa BBI waziri alisema kwamba serikali itafanikisha shughuli hiyo.

"Tutawezesha mchakato wa BBI kama tu vile sisi huwezesha shughuli zingine…Ni jukumu letu, hapatakuwepo wakati ambapo tutahujumu haki za yeyote, ikiwemo haki ya kufanya mikutano," alisema.

Wakati huyo huo waziri aliwahakikishia wakenya kwamba usalama wa kitaifa uko imara na kwamba kila mtu anafaa kuishi bila hofu yoyote.

Waziri aliyasema haya muda mfupi tu baada ya mkuu wa DCI George Kinoti kutangaza kwamba serikali tayari imeanzisha mchakato wa kuhakikisha kwamba wahasiriwa wa machafuko ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007/8 wanapata haki.

Alisema uchunguzi unaendelea kuhusu waliotekeleza dhulma hizo na kwamba tayari wamepata malalamishi zaidi ya 70 kutoka kwa wahasiriwa ambao wako tayari kutoa ushahidii.

Kinoti alikuwa ameonya kwamba kamwe serikali na idara husika za usalama haitakubali tena machafuko na kuruhusu mwanachi yeyote kudhulumiwa kwa sababu yoyote ile.