Itumbi na Matiang'i mahakamani, uamuzi kutolewa Ijumaa

Muhtasari

• Itumbi alisema kwamba ameafikia vigezo kumwezesha kumshtaki Matiang’i.

• Itumbi anataka  Matiang’i kushtakiwa kwa makosa manne kuhusiana na sakata ya Ruaraka.

• Mahakama ilidinda kusikiza mawasilisho ya ofisi ya DPP.

 

Dennis Itumbi (Picha: Maktaba)
Dennis Itumbi (Picha: Maktaba)

Mahakama ya kukabiliana na ufisadi siku ya Ijumaa itatoa uamuzi ikiwa mwanablogi Dennis Itumbi atakubaliwa kumshtaki binafsi waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang’i kuhusu sakata ya ardhi ya Ruaraka.

Itumbi ambaye siku ya Jumanne alifiki mbele ya hakimu Douglass Ogoti alisema kwamba ameafikia vigezo vyote kumwezesha awasilishe kesi ya kibinafsi dhidi ya Matiang’i.

Alipoulizwa ikiwa alikuwa na Ushahidi wa kutosha kumshtaki Matiang’i, alisema: “Nitawasilisha ushahidi wangu ikiwa nitapata idhini ya kuwasilisha kesi…moja wapo wa ushahidi unaohitajika ni taarifa ya mashahidi.”

Wakati huo huo, Ogoti alikataa kusikiza mawasilisho ya ofisi ya mkurugenzi wa mshataka (DPP) akisema kwamba ombi la Itumbi halihitaji mchango wa wahusika katika kesi hiyo.

"Nahitaji kumsikiza Itumbi kwanza ili kuona ikiwa kesi yake inaafikia vigezo vya sheria vinavyohitajika kabla aruhusiwe kumkabidhi stakabdhi za kesi waziri ambaye anataka kumshtaki binafsi," alisema.

Itumbi alisema kwamba aliamua kwenda mahakamani kutokana na utepetevu wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kumshtaki waziri Matiang’i licha ya mahakama kuu kuthibitisha kwamba ardhi hiyo ya Ruaraka ilikuwa ya umma na ilinyakuliwa kinyume cha sharia.

Itumbi anataka waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i kushtakiwa kwa makosa manne kuhusiana na sakata hiyo.

Mashtaka hayo yanajumuisha, matumizi mabaya ya mamlaka, kukosa kufuata sheria za usimamizi wa raslimali za umma, kutekeleza makosa ya kifedha na kushirikiana na wengine kulaghai umma.

Mahakama mwezi Juni mwaka jana iliamua kwamba kipande cha ardhi ambamo shule mbili zimejengwa ni cha umma na kwamba serikali ilipotoshwa na tume ya ardhi nchini kumfidia mfanyibiashara Francis Mburu.

Matiang’i wakati huo alikuwa akihudumu kama waziri wa elimu ingawa sasa  ni waziri wa usalama wa ndani.