Uhuru na Raila kuzindua ukusanyaji wa saini za BBI

Muhtasari

• Zoezi hilo linatarajiwa kuchukuwa siku saba kukamilishwa.

• Uzinduzi huo ulikuwa imepangiwa kufanyika wiki iliyopita lakini ukaahirishwa.

• Linalenga kukusanya saini milioni moja ili kuafikia matakwa ya sheria.

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila. (Picha; MAKTABA)
Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila. (Picha; MAKTABA)

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga leo Jumatano wanazindua zoezi la ukusanyaji saini za kuidhinisha mchakato wa BBI.

Uzinduzi huo ambao unaandaliwa katika jumba la KICC ulikuwa umepangiwa kufanyika Novemba 19, lakini ukaaharishwa kulingana na kile kamati simamizi ilisema ni kuchelewa kukamilishwa kwa mswada husika kufanikisha zoezi hilo.

Makatibu wa kamati maalum inayosimamia zoezi hilo mbunge wa  zamani Dennis Waweru na mbunge wa Suna East Junet Mohamed walisema kwamba shughuli ya ukusanyaji saini inatarajiwa kuchukuwa tu muda wa wiki moja kukamilika.

 

“Tunatoa wito kwa wakenya wenye nia njema, wale wanaotaka kuangamiza ufisadi, ukabila, vitisho, kutengwa kwa baadhi ya maeneo, kuimarisha Maisha ya vijana, wanawake na walemavu kuabiri gari la BBI,” Waweru alisema siku ya Jumatatuu.

Kulingana na kamati inayoongozwa na Waweru na Junet, shughuli ya kukusanya saini milioni moja kutoka kaunti zote 47 itachukuwa tu siku saba.

Wawili hao walikuwa wametoa hakikisho kwamba zoezi hilo litafanyika kuambatana na kanuni na masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Covid-19.